Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amesema mabadiliko ya Sheria za Habari nchini, bado yanahitajika na kudai kuwa kasi ya sasa ya kufanikisha mchakato huo imepungua tofauti na awali.
Balile ameyasema hayo hivi karibuni jijini Dar es Salaam, na kumuomba Waziri wa Habari, Mawasiliasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye kuongeza kasi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Amesema, ukimya uliopo na kasi ndogo ya sasa inatia shaka kukamilika kwa mchakato huo kabla ya kuanza kwa vikao vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la Septemba, 2022.
“Awali tulikwenda vizuri, lakini baada ya Mei 3 mwaka huu (Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani), tunaona kasi imepungua kidogo, awali Wizara ya Habari chini ya Nape, ilipanga kufanya vikao mbalimbali na wadau wa habari, lakini mpaka sasa havijafanyika,” amefafanua Balile.
Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa, “Bado tunazihitaji sheria, bado tunahitaji hayo mabadiliko haraka kadri inavyowezekana kuliko wakati wowote ule kwa sababu, tukipitwa na lile bunge la mwezi wa tisa, ina maana tutasubiri mwaka mmoja baadaye. Bunge la mwezi wa tisa ndio la miswada.”
Hata hivyo, pamoja na mchakato huo kuchelewa Balile amasema iwapo Wizara ya Habari ikiamua kwa dhati kuongeza kasi katika mchakato huo, upo uwezekano wa kufikia malengo ndani ya muda muafaka na kuondoa sintofahamu iliyopo.
Ameongeza kuwa, kiu iliyopo ni uwepo wa haki ya kupata habari na uhuru wa vyombo vya Habari, hali itakayowezesha haki nyingine kama uhuru wa mawazo ikiwemo na mambo mengine yanayolalamikiwa na wadau katika kada mbalimbali nchini.
“Ikiwa uhuru haujalindwa kisheria, basi unachelewesha hivi vingine kupatikana katika jamii na huu ni mjadala na mchakato tunaopaswa kushirikishana tulio wengi kwa Pamoja ili kuleta ufanisi,” amesema.
Akizungumza katika Mkutano wa wadau wa maendeleo wa kusaidia ukuaji wa habari Julai 13, 2022 Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye alisema, serikali imetoa nafasi kwa wanahabari kuwasilisha mbadala wa maoni yao ili kurahisisha malengo ya kuukamilisha mchakato huo.
“Serikali imetoa nafasi kwa wanahabari kuleta mbadala wa yale yanayolalamikiwa, tukae mezani tuzungumze na huo mchakato haiwezi kuwa mfupi, ni chakato wa mazungumzo, mie nimeukuta na tuaendelea nao. Tuna malengo ya kuukamilisha mapema kadri inavyowezekana,” alisema Nape.
Amesema, Sheri ya habari ilipotungwa, ililenga kutatua matatizo ya habari ikiwemo ajira, maslahi, mazingira ya kazi, haki na wajibu wa Waandishi wa Habari na kwamba masuluhisho yaliyopo kwenye sheria, ndio yanayo leta mkanganyiko kwa pande mbili zinazokinzana.
Kwa upande wake Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, alisema serikali imeonesha dhamira ya kutaka kupitia upya sheria na taratibu zote zilizowekwa kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari 2016.