Kocha Mkuu wa Young Africans amesema hajafurahishwa na matokeo ya sare ya bao moja kwa moja dhidi ya Namungo FC, kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uliochezwa juzi Jumapili (Novemba 22) Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam.  

Kaze amesema hawajafurahishwa na matokeo hayo ambayo yamewanyima nafasi ya kuongoza msimamo wa Ligi, lakini bado anahitaji muda wa kuwapa mbinu mpya washambuliaji wake ili kumudu kutumia vema nafasi wanazopata kwa kuvuna idadi kubwa ya mabao.

Amesema bado ana kazi kubwa ya kutafuta njia nyingine ya kuwanoa washambuliaji ili kuweza kupambana na mabeki na hatimaye kucheka na nyavu.

Amesema dakika 45 za kipindi cha kwanza walipata nafasi nyingi za wazi na kupoteza kwa sababu ya washambuliaji wake kutokuwa na purukushani za madhara kwa mabeki wa timu pinzani.

“Kulingana na jinsi safu ya ushambuliaji ilivyo, nahitaji kupata watu, ila sitaweza kuweka wazi kwa sababu nitawavunja moyo wachezaji niliokuwa nao wakati bado tuna michezo sita kabla ya dirisha la usajili kufunguliwa,” amesema Kaze.

Amesema mbali na washambuliaji wake, mapungufu alioyaona ni kwenye safu ya ulinzi kwa kutokujipanga vizuri na wakicheza bila ya maelewano, hivyo kuiruhusu Namungo FC kutumia udhaifu wao kusawazisha muda mfupi baada ya kupata bao.

“Tulikosa mwelekeo baada ya kushindwa kujua tunazuia kuelekea wapi, jambo ambalo limetokea kwenye mechi tatu mfululizo tulizopata sare hivi karibuni, ikiwamo dhidi ya Gwambina, Simba na Namungo, hilo nalo nimeliona naenda kulifanyia kazi,” amesema kaze.

Young Africans kesho itarejea tena dimbani kucheza mchezo wa mzunguuko wa 12 wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Azam FC ambao watakua nyumbani Azam Complex Chamazi, Dar es salaam.

Azam FC wanaongoza msimamo wa Ligi Kuu kwa kumiliki alama 25 na mabao yake 18, ikifuatiwa na Young Africans yenye alama 25 ikiwa imefunga mabao 13, huku SImba SC inashika nafasi ya tatu kwa alama 23.

Kwa hesabu hizo, mshindi atakaepatikana kwenye mchezo wa keshokutwa Jumatano, ataongoza msimamo wa Ligi Kuu kwa tofauti ya alama tatu, lakini matokeo ya sare yataendelea kuibeba Azam FC.

Simba SC safarini Nigeria
Ajali yaua wanane Bukoba

Comments

comments