Aliyewahi kuwa mwamuzi wa kiwango cha juu katika ligi ya nchini Uingereza Keith Hackett amepinga maamuzi ya chama cha soka nchini humo FA ya kumteua mwamuzi Anthony Taylor kuchezesha mchezo wa mwanzoni mwa juma lijalo (Siku ya jumatatu) kati ya Liverpool dhidi ya Manchester United.

Hackett ambaye pia aliwahi kuwa mkuu wa bodi ya waamuzi wa soka nchini Uingereza amesema amestaajabu kuona FA wamevuka mipaka ya kwenda kinyume na uteuzi ambao ulikua umezoeleka siku za nyuma kwa lengo la kutunza heshima ya mchezo wa mahasimu wa ligi ya PL (Liverpool na Man Utd).

Hackett amedai kuwa, Taylor anakosa sifa ya kuchezesha mchezo huo kutokana na mazingira ya makazi yake ambayo yapo karibu na makao makuu ya Man Utd (Old Trafford), jambo ambalo anaamini huenda likaibua shaka miongoni mwa mashabiki wa Liverpool endapo yatajitokeza maamuzi ya utata.

Amesema mwamuzi huyo mwenye umri wa miaka 37, alipaswa kutafutiwa mchezo mwingine wa ligi na sio wa mahasimu wa soka nchini Uingereza ambao mara kadhaa hugubikwa na kadhia mbali mbali kabla na baada ya kuchezwa.

Image result for Anton Taylor Liverpool Vs Man utdAnthony Taylor

Hata hivyo Hackett, amekiri kupendezwa na uchezeshaji wa Taylor kwa kusema siku zote amekua anazingatia uweledi wa hali ya juu, lakini sifa ya makazi yake kuwa umbali wa maili sita kutoka Old Trafford ndio inampa mashaka na kumuhurumia.

“Hakuna ambaye anaweza kuonyesha shaka juu ya uwezo wake wa kuchezesha soka, lakini inawezekana watu wakahoji ukaribu wa kimakazi uliopo baina yake na Old Trafford endapo itajitokeza mambo yanakwenda mrama katika uwanja wa Anfield siku hiyo ya jumatatu.

“Binafsi namkubali sana Taylor na amekua mfano wa kuigwa na waamuzi wengine chipukizi, lakini ninapata mashaka makubwa sana na huenda akajikuta anajiingiza kwenye matatizo kutokana na uteuzi wa FA ambao haukuzingatia vigezo. ” Amesema Hackett alipohojiwa na Sky Sports

Tayari mashabiki wa Liverpool wamekua katika midajala ya kina tangu jana kuhusu uteuzi wa mwamuzi Anton Taylor uliofanywa na FA, na wengi wao wanaamini huenda akawafanyia kusudi kwa kuinyonga timu yao ambayo wamesisitiza ina uwezo mkubwa wa kuifunga Man Utd msimu huu.

Rais Magufuli aagiza viongozi kurudisha fedha za mwaliko wa Mwenge, awataka kutohudhuria
Algeria Wavunja Mkataba Wa Milovan Rajevac