Katika kuendeleza sera ya kubana matumizi na kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa tija, Rais John Magufuli ameagiza viongozi wote wa Serikali waliokuwa wamealikwa kuhudhuria kilele cha mbio za mwenge wa uhuru mkoani Simiyu kutohudhuria.

Rais Magufuli pia ameagiza kuwa viongozi ambao wamelipwa posho za kujikimu kwa ajili ya kuhudhuria sherehe hizo wazirejeshe. Viongozi walioruhusiwa kuhudhuria sherehe hizo ni walio ndani ya mkoa huo pekee.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu, viongozi ambao wametakiwa kufuta safari hiyo ni pamoja na wakuu wote wa mikoa, wakuu wote wa wilaya, Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mtaa, Mameya na wenyeviti wa halmashauri pamoja na watumishi wengine.

Aidha, Rais Magufuli amewataka viongozi hao kubaki katika maeneo yao na kujiwekea utaratibu wa namna bora ya kumuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kwani sherehe za kilele cha mwenge wa uhuru zitafanyika Oktoba 14, siku ambayo Baba Taifa alifariki miaka 17 iliyopita.

Ameagiza halmashauri na miji ambayo mbio za mwenge wa uhuru zilibaini kuwa zilifanya vizuri katika shughuli za maendeleo, zitambuliwe katika sherehe hiyo ambayo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Ali Mohammed Shein.

Sergio Aguero Ashindwa Kutimiza Ahadi
Keith Hackett: FA Wanamtafutia Matatizo Anthony Taylor