Wakili na Mwanaharakati maarufu wa wa Kenya, Dkt. Miguna Miguna amewasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), hii leo Oktoba 20, 2022 akitokea nchini Canada alikokuwa akiishi kwa takribani siku 1,716 (miaka minne), tangu kuondoka jijini Nairobi, huku akisema kilichomtokea hapendi kimtokee mtu mwingine.
Mara baada ya kuwasili, Miguna ambaye anatarajia kuhudhuria sherehe za mashujaa alipokelewa na wafuasi wake na kusema “Nimefurahi sana kurejea nyumbani natoa shukrani zangu kwa Wakenya wote ambao wamesimama nami, kwa muswada wa haki wa katiba na kwa Idara ya Mahakama iliyosimama sheria.”
Hapo jana, (Jumatano Oktoba 19, 2022), Miguna alichapisha katika mtandao wa kijamii picha za barua za mwaliko wa kuhudhuria sherehe za kitaifa za Siku ya Mashujaa katika bustani ya Uhuru Gardens, na baadaye Bustani katika Ikulu ya Nairobi ambapo Oktoba 12, 2022, alifichua kuwa arifa nyekundu alizowekewa zilikuwa zimeondolewa.
Kupitia ukurasa wake wa twitter, Dkt. Miguna alifafanua katika andiko lake alilochapisha kwamba, “Serikali ya Rais wa Kenya, William Ruto na na Makamu wake, Rigathi Gachagua imeondoa arifa Nyekundu, ambazo Uhuru Kenyatta aliweka dhidi yangu na kuwasili kwangu ni hii leo Oktoba 20 majira ya saa kumi na mbili asubuhi.”
Wakili huyo mwenye makao yake nchini Canada, alifukuzwa nchini Kenya kwa mara ya kwanza Februari 6, 2018, baada ya kukamatwa kwa kufuatia kiapo chenye utata cha Januari 30, 2018 cha aliyekuwa mgombea urais wa Muungano wa National Super Alliance, Raila Odinga kama “Rais wa Watu”.
Baada ya kukamatwa, alizuiliwa kwa muda wa siku tano, akihama kati ya vituo vya polisi vya Kiambu na Kajiado kabla ya kufukuzwa nchini humo Februari 6, 2018 licha ya zuio la mahakama dhidi yake na mapema Februari 26, 2018 Jaji Chacha Mwita aliamuru arejeshwe Kenya na kusitisha tamko la Serikali kuwa yeye ni mhamiaji aliyepigwa marufuku.