Huduma ya Kitaifa ya Polisi nchini Kenya (NPS) imesema kuwa uchunguzi umeanza kuhusu vurugu za Bomas, zilizoshuhudiwa Jumatatu, Agosti 15, kabla ya kutangazwa kwa matokeo ya urais.
Utulivu ulirejea baada ya vikosi vya polisi kuwafukuza waandamanaji waliozua ghasia. Katika taarifa siku ya Jumatano, Agosti 17, NPS ilisema tayari kitengo cha uchunguzi kimepokea kamera za CCTV ili kuzikagua na kuzituma kwa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kwa uchunguzi zaidi.
“Katika kisa cha pili kinachohusisha mzozo katika Kituo cha Kitaifa cha Kuhesabu kura cha IEBC-Bomas, polisi wanashughulikia suala hilo na kuendelea na uchunguzi. Faili za CCTV zimekusanywa na kutumwa kwa uchunguzi zaidi wa kitaalamu ili kusaidia uchunguzi,” NPS ilisema na kutoa wito kwa umma kutoa taarifa za siri ambazo zitasaidia katika uchunguzi.
Taarifa hiyo ilikuja saa chache baada ya Chebukati kuwataka maafisa wa polisi kuwakamata waliowashambulia makamishna na maafisa wa tume hiyo katika ukumbi wa Bomas Jumatatu.
Chebukati alisema kuwa makamishna Abdi Guliye na Boya Molu na Afisa Mkuu Mtendaji wa IEBC Marjan Hussein Marjan walipigwa na kujeruhiwa na watu waliokuwa wameandamana na wanasiasa wakati wa shughuli ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa urais.
Mwenyekiti huyo wa IEBC vile vile alilalamikia kile alichokitaja kama vitisho vinavyoelekezwa dhidi ya maafisa wa tume hiyo wakiwa kazini na kutokana na vitisho hivyo, baadhi ya wafanyakazi wa IEBC wameogopa kuripoti kazini wakihofia maisha yao.
“Tume hii inalalamika kuwa wafanyakazi wake ambao walifanya kazi yao kwa kujitolea katika Kituo cha Kitaifa cha kujumlisha kura za urais sasa wanatishwa, kudhulumiwa na hata kukamatwa kiholela. Hali hii inaathiri uhuru wao wa kufanya kazi,” akaongeza.
Agosti 15, kabila ya kutangaza Matokeo ya Urais Nchini Kenya, mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alilazimika kukimbia katika ukumbi wa Bomas of Kenya kwa muda baada ya vurugu kuzuka.