Rais mteule wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud, amemaliza rasmi ziara yake ya kikazi ya siku mbili akiwa nchini Kenya, yenye matarajio ya kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo mbili.
Akiwa nchini humo na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta, pia mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hizo walisema mataifa hayo mawili yamekubali kuanza upya kwa biashara ya mirungi.
Hatua hiyo, inamaanisha kuwa usafirishaji hewa wa mirungi inayojulikana pia kama miraa utaanza tena baada ya kusimama kwa miaka 2.
Somalia ni mojawapo ya soko kubwa la miraa na Kenya ya kati, ambayo ni mzalishaji mkubwa wa mmea huo ambao majani na mashina yake ni kichocheo maarufu na kusababidha hamu ya kula.
Miongoni mwa mikataba mbalimbali iliyotiwa saini na viongozi hao ni ile inayoelekeza upatikanaji wa soko la samaki kutoka Somalia hadi Kenya ikiwemo kukubaliana kupunguza baadhi ya vizuizi vya viza na kufungua tena mipaka.
Rais Kenyatta na Rais Mohamud wameelekeza pia kuharakisha upatikanaji wa soko la haraka la samaki kutoka Somalia hadi Kenya ili kukuza biashara na kufungua fursa za kiuchumi baina ya nchi hizo mbili.