Kesi ya mita 200 iliyofunguliwa na wakili wa Peter Kibatala kwenye mahakama kuu ya Tanzania inatarajiwa kuhitimishwa leo mbele ya jopo la majaji watatu, ambapo jana mvutano mkubwa wa kisheria ulishuhudiwa mahakamani kati ya upande wa mlalamikaji na upande wa serikali ambao ni upande wa utetezi.

Wakili Kibatala aliiomba mahakama hiyo kutoa maana halisi na kusudio la kifungu cha sheria ya uchaguzi namba 104 (1), huku akidai kuwa sheria hiyo inamruhusu mpiga kura mwenye shauku kukaa mita 200 kwa utulivu kufuatilia zoezi zima la uchaguzi.

Pia, Kibatala aliambatanisha makatazo ya NEC na Rais Jakaya Kikwete kuhusu kutokaa kabisa katika eneo la kupigia kura na kurudi nyumbani, akiliomba jopo la majaji hao kutolea maamuzi kama yalikuwa sawa kwa mujibu wa kifungu cha sheria hiyo.

MITA 200

Hata hivyo, baada ya mvutano wa muda mrefu kati ya pande hizo mbili, kauli ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kuwataka wananchi kupiga kura na kisha kukaa mita 200 kwa lengo la kulinda kura zao liliibuka katikati ya mchakato wa kesi hiyo ambapo Jaji Aloysius Mujuliza alitumia kauli hiyo kumbana mlalamikaji.

Jaji Mujuliza: Mbowe alisema wakimza kura wake mita 200, ni weli?

Wakili Kibatala: Ndiyo Mheshimiwa

Jaji Mujuliza: Aliwaambia akina nani?

Wakili Kibatala : Wapiga kura na wafuasi wa chama chake.

Jaji Mujuliza: Wakae ili wafanye nini?

Wakili Kibatala: Walinde kura.

Jaji Mujuliza: Kinacholindwa ni watu, kura au tukio la uchaguzi?

Wakili Kibatala: Mchakato mzima wa uchaguzi.

Ni dhahiri kuwa pamoja na mambo mengine, majibu ya swali hilo yatachangia katika kutoa maamuzi ya mwisho.

Aidha, Wakili Kibatala alidai kuwa haki ya kikatiba haiwezi kuchukuliwa kwa misingi ya madhanio ya kuvunja amani kwakuwa ni kinyume cha sheria.

Suala la kutokuwapo kwa mikutano na mkusanyiko katika siku ya kupiga krua, Wakili Kibatala alidai kuwa mikutano inayozungumziwa kwenye sheria ni mikutano ya kampeni na sio vinginevyo hivyo akaliomba jopo la majaji kutoa maamuzi yanayowapa haki hiyo wapiga kura.

“Endapo mtakubalina nasi kwamba mikutano inayozungumziwa hapa ni ya kisiasa ama kampeni, basi watu kukaa kwa utulivu umbali wa mita 200 kutoka kwenye kituo cha kupigia kura ni haki na haki hiyo haiwezi kuchukuliwa kwa madhanio ama misingi ya woga ua hofu,” alisema Kibala.

Kesi hiyo iliahishwa na imepangwa kutolewa maamuzi mepema leo asubuhi.

 

Baada Ya CCM Kutangaza Safu Ya Wafunga Kampeni, Chadema Yaanza Kutangaza Safu Kuwakabili Mikoani
Neymar Kuwakabili Argentina Pamoja Na Peru