Siku moja baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutangaza mpango wao wa kufunga kampeni kwa kishindo nchi nzima, wahasimu wao kisiasa, Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wameanza kutaja majina ya safu yake ya kampeni itakayowakibili katika mikoa husika.

Moja kati ya majina yaliyotajwa na Chadema, ni jina la mzee Kingunge Ngombale Mwiru, atakayehudhuria ufungaji wa kampeni katika mkoa wa Mara ambapo CCM wamemtaja Jaji Mstaafu, Joseph Warioba kufunga kampeni za chama hicho Mkoani humo.

Jaji Joseph Warioba atahudhuria ufungaji wa kampeni na kumnadi mgombea wa jimbo la Musoma Mjini, David Mathayo pamoja na wabunge wengine wa Mara, huku Mzee Kingunge Ngombale Mwiru atakuwa akimnadi mgombea wa Jimbo la Musoma Mjini, Vicent Nyerere na wagombea wengine wa ubunge wa majimbo ya mkoa huo.

Jaji Joseph Warioba (Katikati) akimnadi mgombea ubunge jimbo la Kawe, Kippi Warioba

Jaji Joseph Warioba (Katikati) akimnadi mgombea ubunge jimbo la Kawe, Kippi Warioba

Mzee Kingunge Ngombale Mwiru akiongea na wananchi

Mzee Kingunge Ngombale Mwiru akiongea na wananchi

Aidha, Wakati CCM watakuwa wakifunga kampeni zao kesho jijini Mwanza kwa mkutano mkubwa zaidi ukiwa na mgombea urais wa chama hicho, Dkt. John Magufuli, mkutano utakaohudhuriwa na mwenyekiti wa chama hicho, Jakaya Kikwete, Chadema watakuwa wakifunga kampeni zao za ubunge kwa kufanya mkutano mkubwa utakaohudhuriwa na Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye na wagombea ubunge wote wa majimbo ya Mwanza Mjini.

Aidha, Chadema watakuwa na mkutano mkubwa wa kufunga kampeni kitaifa kesho, ambapo mgombea wake wa urais, Edward Lowassa na viongozi wengine wa Ukawa watakuwa katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, CCM wameonekana kuwafunika Chadema kwenye vyombo vya habari vinavyotarajiwa kurusha moja kwa moja mikutano ya kufunga kampeni.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Mjumbe wa kamati ya kampeni ya CCM, January Makamba alitangaza mkakati wa kihistoria wa kurusha matangazo moja kwa moja kuonesha mikutano yote mitano kutumia vituo vitano vikubwa vya runinga pamoja na vituo vya radio 67.

Hii ni safu ya makada wakongwe wa CCM watakaofunga kampeni kwa kishindo kwenye mikoa 7 nchini na kufanya mikutano mikubwa.

  1. Mwanza – Ndugu Jakaya Mrisho Kikwete, Mwenyekiti wa CCM, Dkt. John Pombe Magufuli, Mgombea Urais, na Ndugu Samia Hassan Suluhu, Mgombea Makamu wa Rais
  2. Tanga – Ndugu Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu wa CCM
  3. Mbeya – Ndugu Benjamin William Mkapa, Mwenyekiti wa CCM Mstaafu
  4. Mtwara – Ndugu Ali Hassan Mwinyi, Mwenyekiti wa CCM Mstaafu
  5. Kigoma – Ndugu Philip Mangula, Makamu Mwenyekiti wa CCM
  6. Kilimanjaro – Ndugu Yusuf Makamba, Katibu Mkuu wa CCM Mstaafu
  7. Mara – Ndugu Joseph Warioba, Mjumbe wa Kamati Kuu na Waziri Mkuu Mstaafu

 

Lowassa kulihutubia Taifa Leo Usiku, Ajihakikishia Ushindi Mkubwa
Kesi Ya Mita 200: Swali La Jaji Kwa Wakili Kibatala Lamgusa Mbowe