Baada ya kifo cha aliyekuwa mchezaji wa klabu ya Mtibwa Sugar Iddi Mobby ,klabu na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) zimeshauriwa kuwapima wachezaji afya kabla ya kuanza msimu na kila mara lengo likiwa ni kujua afya zao.

Mobby alifariki Machi 5 mwaka huu katika hospitali ya Benjamini Mkapa Jijini Dodoma alipokuwa akipatiwa matibabu na mwili wake ulisafirishwa mjini Shinyanga na kuzikwa Machi 7, mwaka huu.

Idaiwa mchezaji huyo alijisikia vibaya Machi 5 mwaka hu Turiani mkoani Morogoro, wakati akifanya mazoezi ya kukimbia barabarani na alipelekwa katika hospitali ya Misheni na baadae Benjamini Mkapa, umauti ulipomkuta.

Daktari bingwa wa mifupa na majeraha kutoka Hospitali ya Benjamini Mkapa, Alfred Amede alishauri mwanzo wa msimu klabu kuhakikisha zinawafanyia uchunguzi wa kina wachezaji wao.

“Ikiwemo kufanya baadhi ya vipimo kama vya moyo, ini figo ili kuweza kujua afya zao, baadhi ya timu zinafanya lakini kuna timu hazifanyi,”alisema Dk Amede.

Dk Amede ambaye pia ni daktari wa timu za vijana za Taifa, U17, 20 na 23, alisema pia kunatakiwa kuwe na uchunguzi wa mara kwa mara wakati ligi ikiendelea ili kujikinga na matatizo pindi mchezaji anapopata shida.

“Ni jukumu la TFF na klabu kuhakikisha zinakuwa na wataalamu sahihi ili uchunguzi utakaofanywa uwe sahihi. Wachezaji wapate bima nadhani kuna mkataba ulisainiwa lakini hili nalo ni muhimu kwa sababu haya matibabu ni gharama.”

Daktari huyo bingwa wa mifupa na majeraha alishauri pia kuwe na vyumba maalum katika viwanja wa mazoezi ambavyo vitasaidia pindi mchezaji anapopata tatizo.

“Ikiwezekana klabu zisiruhuwisi kutumia viwanja ambavyo havina vyumba ya dharura hili tulipe kipaumbele kwa sababu hili ni muhimu sana,” alisema Dk Amede.

Chanzo: Mwanaspoti

Ally Mayay atoboa Jumuiya ya Madola
Mwinyi Zahera ajitia kitanzi Polisi Tanzania