Mlinzi wa Kulia wa kikosi cha Simba SC Shomari Kapombe ameweka wazi kuwa kinachomfanya awe bora kila awapo uwanjani ni kutanguliza malengo ya timu kisha yeye anafuata.

Nyota huyo ni chaguo la kwanza kwenye kikosi cha Simba SC kinachonolewa na Kocha Mkuu, Roberto Oliveira raia wa Brazil.

Kwenye Michezo 19 ya Ligi Kuu, Kapombe ameyeyusha dakika 1,686 huku akitoa jumla ya pasi tano za mabao na kutupia kambani mabao mawili.

Kapombe amesema kuwa, kila mashindano ambayo wanashiriki yana umuhimu kwao na wanapambana kufanya vizuri.

“Tunamshukuru Mungu kwa kuwa tumekuwa tukipata matokeo kwenye mechi ambazo tunacheza na kikubwa kwangu mimi ambacho huwa ninatazama ni malengo ya timu kuona yanatimia.”

“Ikiwa malengo ya timu yatatimia inamaanisha kwamba nasi tutafikia malengo yale ya mchezaji mmoja mmoja ndio maana kila mchezaji anaonyesha ushirikiano kwa wachezaji wenzake kwa kuwa sisi ni timu,” amesema Kapombe.

Kapombe anatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi cha SImba SC kitakachopambana na Mtibwa Sugar baadae leo Jumamosi (Machi 11), katika Uwanja wa Manungu Complex mkoani Morogoro.

Mwinyi Zahera ajitia kitanzi Polisi Tanzania
Prisons yatamba kuchukua alama tatu Lindi