Mabingwa wa soka nchini Rwanda, (Armée Patriotique Rwandaise) APR, wanatarajiwa kuwasili jijini Dar es salaam hii leo jioni, tayari kwa mchezo wa mkondo wa pili wa ligi ya mabingwa barani Afrika dhidi ya Young Africans, utakaochezwa mwishoni mwa juma hili.

APR, watatua nchini, huku wakiwa na kumbukumbu mbaya ya kukubali kufungwa katika uwanja wao wa nyumbani wa Amahoro, mabao mawili kwa moja mwishoni mwa juma lililopita, hali ambayo inachukuliwa kama sehemu ya kuongeza chachu ya mpambano utakaochezwa hapa nchini siku ya jumamosi.

Taarifa kutoka mjini Kigali zinaeleza kwamba kikosi cha APR, kitaondoka mjini humo mishale ya saa saba mchana na kutarajia kuwasili jijini Dar es salaam saa tatu baadae.

Kikosi cha wanyarwanda hao kilifanya mazoezi yake ya mwisho jana katika viwanja vya Kicukiro na bahati nzuri kwao ni kwamba, mshambuliaji wao hatari, Issa Bigirimana aliyekosa mchezo wa kwanza amerudi.

Bigirimana aliyekosa mchezo huo kutokana na kuwa kwenye msiba wa mama yake mzazi, jana amefanya mazoezi kikamilifu na wenzake na atasafiri na timu kuja Dar.

Bahati mbaya kwao APR, beki Ngabo Albert ataendelea kuwa nje kwa sababu ya maumivu sawa na mshambuliaji Michel Ndahinduka anayesumbuliwa na maumivu ya nyama za paja.

Kocha Nizar Khanfir aliwaambia Waandishi wa Habari jana kwamba anataka kuimarisha safu yake ya ushambuliaji kwa kumuanzisha Bigirimana Jumamosi.

“Tunaendelea kurekebisha baadhi ya makosa, katika soka kila siku unajifunza kitu kipya. Kikubwa kwetu ni maandalizi ili kushinda kila mechi tunayocheza,”amesema.

Kwa ujumla kocha huyo anatarajiwa kufanya mabadiliko mawili kutoka kikosi cha mechi ya kwanza, Bigirimana akichukua nafasi ya Mubumbyi na Benedata akichukua nafasi ya mpwa wa kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima, Djihad.

Milutin Sredojevic ‘Micho’ Amjumuisha Kikosini Okwi
Kombe La Dunia Mwaka 2010, Afrika Kusini Yaingizwa Kikaangoni