Shirikisho la soka duniani FIFA limeishtumu Afrika Kusini kwa kulipa hongo ya dola milioni 10 ili kupewa fursa ya kuandaa fainali za kombe la dunia za mwaka 2010.

Kwa mujibu wa ripoti ya gazeti la Telegraph nchini Uingereza, FIFA ilitoa ”taarifa ya mwathiriwa” na ”ombi la kurudisha fedha” hizo kwa afisi ya wakili wa Marekani.

Maafisa wa Afrika Kusini wamesisitiza kuwa hawakulipa hongo.

FIFA inajaribu kukomboa makumi ya mamilioni ya fedha zilizochukuliwa kinyume cha sheria na wanachama wa shirikisho hilo pamoja na mashirika mengine ya soka.

Maafisa wa zamani wa shirikisho hilo lenye dhamana ya mchezo wa soka duniani kote, Chuck Blazer, Jack Warner pamoja na Jeffery Webb ni miongoni mwa wale waliofunguliwa mashtaka huku FIFA ikiwasilisha stakhabadhi kwa mamlaka za Marekani.

FIFA imekuwa katika mgogoro tangu madai ya ufisadi kugunduliwa mnamo mwezi Mei 2015.

Kwa jumla watu 41 pamoja na kampuni kadhaa zimeshtakiwa na mamlaka za Marekani.

Uchunguzi wa Marekani ulifichua ufisadi mkubwa katika shirikisho hilo na FIFA inakadiria mamilioni ya madola yaliibwa kupitia hongo, kiinua mgongo na mipango ya ufisadi iliofanywa na washtakiwa.

Kikosi Cha Armée Patriotique Rwandaise Kuwasili Leo
Wenger Aridhika Na Kiwango Cha Arsenal Dhidi Ya Barca