Baada ya kupokea kisago cha mabao matatu kwa moja, katika mchezo wa mkondo wa pili wa hatua ya 16 bora wa ligi ya mabingwa barani Ulaya, dhidi ya FC Barcelona, meneja wa Arsenal, Arsene Wenger anaamini kikosi chake kilicheza vizuri katika uwanja wa Camp Nou.

Wenger, amejinasibu kwa kuamini hivyo, kutokana na hali ya mvutano wa ushindani ulioonekana wakati wote wa dakika 90, japo mambo yaliwaendea kombo kwa kukubali kufungwa na mashujaa watatu wa Barca, Neymar, Luis Suarez na Messi huku bao la kufutia machozi la The Gunners likifungwa na kiungo kutoka nchini Misri, Mohamed Elneny.

Wenger, amesema hadhani kama kuna mtu anaweza kujitokeza hadharani na kueleza kama walicheza vibaya dhidi ya Barcelona, kutokana na mambo yalivyokenda tofauti na mchezo huo ulivyokua ukizungumzwa kabla ya timu kuingia uwanjani.

“Nafikiri tulicheza vyema, ulikuwa mchezo mzuri kati ya timu mbili nzuri. Tumeondolewa kwa masikitiko lakini wana ustadi wa hali ya juu hasa katika safu ya mashambulizi na ukifanya kosa kidogo tu safu yako ya ulinzi wanaweza kukuadhibu,” alisema Wenger baada ya mchezo.

“Wakati muhimu katika mchezo huo ni mambo yalipokuwa 1-1 kwa sababu nilidhani walikuwa wanayumbayumba kiasi, kama tungefunga bao la pili wakati huo basi mambo yangekuwa tofauti, lakini hatukuweza.

“Katika michezo yote miwili, ukiangalia nafasi ambazo tuliunda, zilikuwa nyingi. inauma kuondolewa kwenye michuano lakini tulicheza vyema sana dhidi ya timu ambayo labda ndiyo bora zaidi Ulaya.”

Arsenal wametupwa nje ya michuano hiyo kwa jumla ya mabao matano kwa moja, baada ya kukubali kupoteza mchezo wa mkondo wa kwanza kwa kufungwa mabao mawili kwa sifuri.

Kwa mantiki hiyo sasa, Arsenal wanaendelea kusota kwa kushindwa kuvuka hatua ya 16 bora ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya, kwani tangu mwaka 2010 hawajawahi kutinga katika hatua ya robo fainali.

 

Hatua ya kuondolewa kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya, inaipa Arsenal nafasi ya kugeuzia nguvu zao kwenye ligi ya nchini England, ambapo mwishoni m wa juma hili watasafiri kuelekea Goodson Park, kwa ajili ya kupambana na Everton.

Arsenal wapo katika mbio za kuwania ubingwa wa nchini England, japo wana tofauti ya point 11 dhidi ya vinara wa msimamo wa ligi hiyo Leicester City.

Kombe La Dunia Mwaka 2010, Afrika Kusini Yaingizwa Kikaangoni
Makala: Bahasha yenye jina la 'Lady Jay Dee' ilisahaulika kwenye tuzo za 'Malkia wa Nguvu?