Wananchi wa Kijiji cha Uhambingeto, Wilayani Kilolo wameangua kilio mbele ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Daniel Chongolo baada ya mradi wa maji kusuasua licha ya mkandarasi anayejenga mradi huo kulipwa.
Baada ya kusikia malalamiko hayo, Chongolo ametoa siku 10 kwa Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kufika Kijiji cha Uhambingeto, Jimbo la Kilolo ambako mradi wa maji umekwama, licha ya Mkandarasi kulipwa zaidi ya asilimia 50, huku zikiwa zimebaki siku chache mkata wa ujenzi kukamilika.
Mradi wa Maji Uhambingeto Kilolo unatekelezwa na Mkandarasi Mshamind Co LTD, kwa gharama ya Sh2.1 Bilioni huku 1.3 Bilioni zikiwa zimekabidhiwa, huku Chongolo akisema haiwezekani fedha itolewe na mradi huo ushindwe kukamilika wakati wananchi wanahitaji maji.
“Waziri wa Maji afike Uhambingeto ndani ya siku 10, aje atoe pole kwa wananchi kwa kuchelewa kwa mradi huu lakini pia atengeneze utaratibu wa wananchi wapate maji, nataka inapofika Septemba 30, wananchi wa Uhambingeto wawe wamepata maji,” alisema Chongolo.
Aidha ameongeza kuwa, “sijaridhishwa na huu mradi, hatuwezi kwenda namna hii, hapa tatizo nimkandarasi twende tukakae tuchukue hatua. Cha msingi hapa ni maji,” amesisitiza Chongolo.
Chongolo akiambatana na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi na Katibu wa NEC, Oganaizesheni Issa Haji Gavu, wapo Iringa kwa ziara ya kukagua utelekezaji wa Ilani, kuhamasisha Uhai wa Chama pamoja na kusikiliza na kutatua kero za wananchi.