Hatimae kocha mkuu wa Namungo FC Thierry Hitimana wamefunguka na kueleza kwa undani kinachoisumbua timu yake, ambayo tayari imeshapoteza michezo miwili kati ya mitatu ya Ligi Kuu Tanzania Bara, msimu huu 2020/21.
Namungo FC ilipoteza mchezo wa pili mfululizo Jumamosi, Septemba 19 mjini Rukwa mkoani Sumbawanga kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, kwa kufungwa bao moja kwa sifuri na maafande wa Magereza (Tanzania Prisons).
Kabla ya hapo walikubali kupoteza nyumbani mkoani Lindi, kwa kufungwa bao moja kwa sifuri na maafande wa Jeshi la Polisi (Polisi Tanzania FC).
Kocha Hitimana, amesema kinachoisumbua timu yake ni kukosekana kwa muunganiko mzuri wa wachezaji wapya na wa zamani, jambo ambalo limepelekea kupoteza michezo hiyo miwili.
Amesema anasikitika kuona amepoteza alama sita ambazo alizihitaji katika michezo hiyo ya mwanzoni mwa ligi, lakini akaahidi kuendelea kuzifanyia kazi changamoto zilizoonekana kikosini kwake.
“Wachezaji wamekuwa wakifanya makosa yale yale, na hali hii ya kurudia makosa inasababishwa na kutokuwa na muunganiko mzuri, ninaendelea kulifanyia kazi ili kupata matokeo mazuri katika mechi zinazofuata,” amesema Hitimana.
Katika hatua nyingine kocha huyo kutoka nchini Burundi, amesema tatizo lingine kikosini kwake ni washambuliaji wake kutokuwa makini na kupoteza nafasi za kufunga zilizotengenezwa.
“Tumepoteza alama nyumbani na ugenini, ukiiangalia mchezo, utaona tumepata nafasi nyingi ila hatukutumia vyema nafasi tulizopata, nimeanza kulifanyia kazi kuhakikisha tunaingia imara zaidi tutakapocheza dhidi ya Mbeya City,” amesema Hitimana.
Namungo walianza vizuri msimu huu kwa kuifunga Coastal Union bao moja kwa sifuri, Septemba 06 Uwanja wa Majaliwa mjini Ruangwa mkoani Lindi.
Mwishoni mwa juma hili Namungo FC watacheza dhidi ya Mbeya City katika mchezo wa mzunguuko wanne utakaochezwa Septemba 25, kwenye Uwanja wa Sokoine jijini, Mbeya.