Walimu tisa wa shule za msingi wilayani Bahi wamefukuzwa kazi kutokana na utoro huku wanafunzi sita wakishindwa kumaliza elimu ya msingi kutokana na mimba.
Ofisa elimu na taaluma wilayani humo, Issa Nchila ametoa taarifa hiyo leo Jumatano kwenye kikao cha wadau wa elimu waliokutana kujadili changamoto zinazosababisha wilaya hiyo kuendelea kushuka kielimu.
Nchila amesema walimu hao walikuwa miongoni mwa walimu 11 waliokuwa wameshtakiwa kwa makosa mbalimbali ya utoro na nidhamu kazini.
Amesema walimu wawili kati ya hao, walishushwa vyeo ikiwemo kupunguziwa mishahara yao.
Ofisa huyo amekiri hali mbaya kwa matokeo ya elimu huku wilaya ikiwa imeshika nafasi ya tano katika halmashauri 8 za Mkoa wa Dodoma.
“Bado tutaendelea kuwachukulia hatua kali kwa kushirikiana na TSD ili kukomesha vitendo hivyo kwani ni moja ya mambo yanayotukwamisha na kufanya watoto wetu wafanye vibaya,” amesema Nchila.
Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Elizabeth Kitundu amesema wilaya hiyo ina tatizo la mimba kwa shule za msingi na sekondari ambalo watalikomesha.