Lugha ya Kiswahili imechaguliwa kuwa lugha rasmi kutumika katika mikutano yote itakayoendeshwa na Umoja wa Nchi za Afrika (AU).
Akiongea na waandishi wa habari katika maadhimisho ya Siku Umoja wa Afrika, yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC),
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amesema kuwa nchi wanachama wa umoja huo zimekubaliana kutumia lugha ya Kiswahili kuendeshea mikutano yake yote.
“Kwa mara ya kwanza katika historia ya Afrika Kiswahili kama lugha halisi mojawapo ya kiafrika kimechaguliwa kuwa lugha rasmi itakayotumika katika mikutano yote ya Umoja wa Afrika ambapo siku za nyuma Kiswahili kilikuwa kinatumika kama lugha ya kazi na katika ngazi ya Mikutano ya Maraisi tu. Jambo hili ni la kujivunia kwa sisi Watanzania na Afrika kwa ujumla”, amesema Mulamula.
Uamuzi wa kukichagua Kiswahili umeenda sambamba na utekelezaji wa kauli mbiu ya maadhimisho ya siku hiyo kwa mwaka huu inayosema ‘Sanaa, Utamaduni na Urithi njia za Kuijenga Afrika tunayoitaka’.