Baada ya kuwasili Dar es salaam jana Jumapili (Septemba 11) sambamba na kikosi chake, Kocha Mkuu wa Muda wa Simba SC Juma Mgunda amesema ana kazi kubwa ya kufanya kuelekea mchezo wa Mkondo wa Pili wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Mabingwa wa Malawi Nyasa Big Bullet.

Simba SC Jumamosi (Septemba 10) iliibuka na ushindi wa 2-0 ugenini na kujiweka katika mazingira mazuri kuelekea mchezo wa Mkondo wa Pili ambao utapigwa jijini Dar es salaam, Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Mgunda aliyekabidhiwa kijiti cha kuliongoza Benchi la Ufundi baada ya kuondoka kwa Kocha Zoran Maki, amesema mchezo bado haujaisha, hivyo atahakikisha anakiandaa vizuri kikosi chake ili kuendelea na mpango wa ushindi.

Amesema Nyassa Big Bullet nao wanaamini mchezo haujaisha, hivyo watakuja Dar es salaam wakiwa na malengo ya kupambana kama walivyofanya kwao katika kipindi cha pili kabla ya Mshambuliaji John Bocco hajafunga bao la Pili na la ushindi.

“Haijaisha hadi iishe, siri ya ushindi huu ni ushirikiano kwa Benchi la Ufundi, Matola amenisaidia sana kunipa mwelekeo, kazi haijaisha tunasubiri mchezo ujao ijayo ili tufanye vizuri tena,”

“Wapinzani wetu watakuja kucheza kwa juhudi zote kwa sababu wanajua ndio nafasi iliyobaki kwao, tunalifahamu hilo tutahakikisha tunaendeleza pale tulipoishia, kikubwa ninaomba ushirikiano kutoka kwa Mashabiki ambao siku zote wamekua msaada mkubwa kwa timu ya Simba SC.”

Kuhusu kasi ya Mshambuliaji Phiri, Mgunda amesema Nyota huyo amesajiliwa kuja kufanya kazi na anachokifanya ni kutimiza wajibu wake, kila anapopewa nafasi ya kucheza.

“Kazi yake ni kufunga ndicho kimemleta Simba, hiki anachokifanya ndio jukumu lake” amesema Kocha huyo wa zamani wa Coastal Union.

Katika mchezo wa Mkondo wa Pili, Simba SC italazimika kusaka ushindi mwingine ama kutoka sare ili kujihakikishia nafasi ya kutinga hatua inayofuata ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, huku Nyassa Big Bullet wakitakiwa kushinda mabao matatu kwa sifuri ama zaidi.

Rais Samia: Uwanja wa Majaliwa utakuwa chachu ya kukuza sekta ya michezo
Waziri amsimamishwa kazi Meneja RUWASA