Serikali ya Jamhuri ya Korea imeipatia Tanzania mkopo wa gharama nafuu wa shilingi bilioni 310 kwa ajili ya upanuzi wa mfumo wa utambuzi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) pamoja na uendelezaji na utunzaji wa mfumo wa taarifa za ardhi.

Mkataba wa awamu ya pili ya mradi wa upanuzi wa mfumo wa utambuzi wa NIDA una thamani ya shilingi bilioni 161 na mkataba wa uendelezaji na utunzaji wa mfumo wa taarifa za ardhi ambao una thamani ya shilingi bilioni 149.

Akizungumza wakati wa halfa hiyo ambayo ambayo pia ilishuhudiwa na Waziri Mkuu wa Korea Han Duck-Soo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa Tanzania na Korea zinajivunia mahusiano yaliyodumu kwa miaka 30 ambayo yamekuwa chachu katika kukuza uchumi wa nchi hizo mbili katika sekta mbalimbali.

“Tunaishukuru sana Korea Kusini kwa kuwa miongoni mwa mataifa yanayoshiriki katika kutatua changamoto za kimaendeleo ikiwemo kupitia Mfuko wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo wa Korea (EDCF)”

Waziri Mkuu amesema kuwa pamoja na mikopo kupitia mfuko wa EDCF, Tanzania pia imekuwa mnufaika wa mikopo kupitia Shirika la Maendeleo la Korea (KOICA). “Tunaishukuru sana Jamhuri ya Korea kwa kutambua kuwa Tanzania ni nchi ya kipaumbele.”

Majaliwa amesema misaada ya KOICA kwenye eneo la afya, elimu ya ufundi, ufadhili wa masomo imesaidia sana kuleta nguvu na msukumo katika kuongeza kasi ya maendeleo ndani ya Serikali.

Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba amesema kuwa mkataba wa awamu ya pili wa mradi wa upanuzi wa mfumo wa utambuzi wa NIDA utaiwezesha mamlaka hiyo kuongeza uwezo wa kutengeneza vitambulisho vya Taifa pamoja na kutunza takwimu. “Mkopo huu utaisaidia NIDA kujikita katika maeneo ya vijijini na kuongeza kasi ya usajili wa vitambulisho.”

“Tunaamini utaratibu huu mpya utaleta urahisi na utaondoa changamoto mbalimbali zilizokuwa zinatokana na kutokuwepo kwa mfumo rahisi na mzuri wa uhifadhi wa taarifa.”

Viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk, Balozi wa Tanzania Nchini Korea Kusini, Balozi Togolani Mavura, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar, Aboud Hassan Mwinyi na watendaji wengine wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Jeshi la Polisi limekamata watuhumiwa 1,212 wa dawa za kulevya
Kongamano la kutatua changamoto za utoaji huduma za mawasiliano