Rais Uhuru Kenyatta ameendelea kukabiliana na makombora ya Naibu wake William Ruto kwa kumshutumu Ruto kutumia uongo na matusi katika azma yake ya kutafuta urais.
Akizungumza siku ya Ijumaa, Julai 8, wakati akiwakaribisha makasisi ndani ya Ikulu ya Nairobi, rais Kenyatta alimkashifu naibu wake, kwa kusema anatumia uwongo na matusi katika harakati zake za kuwania wadhifa wa juu zaidi nchini.
Rais Kenyatta alisema, “baadhi ya wanasiasa walikuwa wakishiriki katika kampeni za udanganyifu, migawanyiko na kupotosha wananchi ili kushinda.”
Viongozi hao, siku za hivi karibuni wamegeukia kampeni ya mizengwe hadharani kufuatia malumbano yao ya kisiasa na kiuongozi ambayo yamechukua miaka mingi.
Naibu Raisi Ruto amekuwa akimlaumu Uhuru kwa kumtenga kutoka serikalini na kupuuza ajenda nne kuu ambazo walikuwa nazo kwa maslahi ya nchi wakati wakitafuta kura 2017.
Kulingana na Ruto, serikali ya Jubilee ilikosea katika muhula wake wa pili kutokana na usitishaji wa vita baina ya Uhuru na kiongozi wa ODM, alisema, “rais aligeukia agenda zingine zisizokuwa za maana.”
Hata hivyo, kwa upande wake rais Kenyatta ameshikilia kuwa mapatano yake na Raila yalikuwa muafaka kwani amani ya taifa ilikuwa inaelekea kusambaratika kufuatia mzozo wa uchaguzi wa 2017.
Rais Kenyatta alisisitiza umuhimu wa amani, umoja na mshikamano katika kilele cha kampeni za kisiasa uchaguzi wa Agosti 9 unaponusia.
“Huna haki ya kusaka uongozi kupitia uongo, matusi na wizi, tayari umeanzisha propaganda na unazunguka nchi nzima ukisema umedhulumiwa. Mkataba ni kati ya watu wawili. Nikikosea wewe pia unakosea. Huna haki ya kutafuta uongozi kwa kusema uwongo, matusi na wizi,” alisema Uhuru.
Wakati huo huo, Rais Uhuru alidokeza kuwa kiongozi wa chama cha Narc Kenya Martha Karua anatosha kuwa mrithi wake kama kiongozi wa eneo lenye wakazi wengi Mlima Kenya.
Kwa upande wa Naibu rais William Ruto kwa sasa hahudhurii kikao cha usalama kuhusu taifa maarufu kama National Security Council.
NSC ndicho kikao muhimu kuhusu usalama wa taifa ambapo rais hukutana na makamanda muhimu katika sekta ya usalama lakini DP Ruto anasema aliwekwa nje ya kikao hicho miaka mitatu iliyopita na sasa ni vigumu kwake kushawishi hatua za kiusalama.
DP Ruto alieleza kuwa alivumilia fedheha nyingi tangu kuibuka kwa mzozo wake na Uhuru, na kuongeza kuwa ingekuwa ni kiongozi wa ODM Raila Odinga au Martha Karua wa Narc Kenya, wangechukua hatua kali.
Duru za kisiasa zinasema kuwa urafiki wa wawili hao wa awali ambao uliwafanya kuchukua uongozi wa nchi 2013 ulififia 2018 wakati rais Kenyatta alipoamua kumrushia ndoano Raila Odinga.