Na Zaka Zakazi

Habari kubwa kwenye ulimwengu wa soka siku za hivi karibuni ni kuibuka kwa kinda la Manchester United, Marcus Rashford.

Chipukizi huyu mwenye miaka 18, aliibuka ghafla kutoka akademi ya United na kufunga mabao manne kwenye mechi mbili muhimu. Hii imekuja baada ya kuacha gumzo kwenye ligi ya vijana wa chini ya miaka 18 ambapo aliibuka mfungaji bora. Baada ya hapo, akarudi shule kufanya mitihani.

Mkasa kama huu ulitokea hapa Tanzania mwaka 1992 kwa Edibily Jonas Lunyamila. Chipukizi huyo wa ajabu alikuwa akisoma shule ya sekondari Buhangija huko Shinyanga huku akiichezea klabu ya Biashara Shinyanga iliyokuwa ikishiriki ligi kuu(daraja la kwanza wakati huo).

Hii ilikuja baada ya  kutoka kuacha gumzo kwenye UMISETA 1992 iliyofanyika Zanzibar. Baada ya hapo Lunyamila alirudi shule kufanya mitihani.

Mwaka huo CECAFA Senior Challenge Cup ilifanyika Tanzania.
CECAFA kama wenye mashindano na FAT (siku hizi TFF) kama wenyeji walipanga kuwe na vituo viwili; Mwanza na Arusha.

Tanzania kama mwenyeki ilipewa nafasi ya mbili; timu A ikaitwa Victoria, iliyokuwa kituo cha Mwanza na timu B ikaitwa Kakakuona ikapangiwa kituo cha Arusha.

Kocha wa Victoria, Paul West Gwivaha, alimtaka chipukizi Lunyamila kwenye timu yake hivyo mmoja wa wafadhili(Abbas Gulamali) alikwenda Shinyanga na gari lake aina ya Shangingi na kukaa nje ya mlango wa chumba cha darasa kumsubiri Lunyamila amalize mitihani ili aondoke naye kwenda Mwanza kujiunga na timu.

Lunyamila aling’aa na Victoria japo ilitolewa kwenye robo fainali kwa kipigo cha 2-1 kutoka kwa Zambia(KK Eleven-iliyopata ajali mbaya ya ndege 1993). Bao pekee la Victoria lilifungwa na Lunyamila.

Safari ya Lunyamila iliendelea na mwaka huo huo akajiunga na Yanga ambayo 1993 aliisaidia kutwaa kombe la klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati huko Uganda huku akifunga bao la ushindi wa 2-1 mbele ya wenyeji SC Villa Jogoo. Lunyamila aliacha gumzo jijini Kampala na hata mabasi mengi yaliandikwa jina lake.

Magufuli apitisha 'fagio' mabilioni ya Benki Kuu
Vicent Bossou Atemwa Kikosi Cha Togo