Mawakili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), jana walishindwa kwa mara nyingine kupata dhamana ya mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, baada ya Mahakama Kuu kutupilia mbali maombi yao.

Mahakama Kuu ilitupilia mbali maombi ya marejeo ya kesi inayomkabili Lema baada ya kukubaliana na hoja zilizowasilishwa na upande wa Jamhuri kuwa marejeo hayo hayana msingi.

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Sekela Moshi alisema kuwa hakukuwa na hoja ya msingi kwa Lema kudai marejeo ya kesi yake badala yake alipaswa kukata rufaa.

Jaji Moshi alieleza kuwa dhamana ya Lema iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi ilizuiwa kutokana na notisi ya maneno iliyowasilishwa na upande wa mawakili wa Jamhuri.

Alisema kuwa vifungu vya 148 hadi 160 vinatoa haki ya dhamana lakini kifungu cha 161 kinaeleza jinsi ambavyo utaratibu huo unaweza kufuatwa bila kuathiri masharti ya kisheria.

Mawakili wa Lema wakiongozwa na Peter Kibatala waliamua kukata rufaa chini ya hati ya dharura baada ya Mahakama kutoa uamuzi huo. Lema alirudishwa tena mahabusu akikabiliwa na kesi ya uchochezi dhidi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli.

CAF Yawapeleka Jela Waamuzi Wa Soka
Chadema kuhakiki wanachama, yajipanga kupunguza kutegemea ruzuku