Kushindwa kwa Kiongozi anayeondoka madarakani nchini Liberia, George Weah sasa kunaweka somo kwa Mataifa ya Afrika juu ya nguvu ya wapiga kura wanakitaka kwa kuwa yeye anakuwa Rais wa kwanza kushindwa katika kinyang’anyiro cha kuwania muhula wa pili wa kusalia madarakani.
Weah ambaye ni maarufu Duniani kwa usakataji wa kabumbu kimataifa, aliingia madarakani mwaka 2018 kwa muhula wa kwanza na alikuwa akitarajia kuendelea na awamu ya pili mwaka huu kabla ya kubwagwa na mpinzani wake, Joseph Bokai katika uchaguzi wa marudio uliokamilika.
Bokai alipata ushindi wa asilimia 50.89 ya kura dhidi ya asilimia 49.11 alizopata Weah ikiwa ni takriban kura zote zilizohesabiwa, ambapo Bokai alimzidi Weah kwa kura 28,000 huku takwimu hizo zikionesha jinsi mchuano wa wawili hao ulivyokuwa mkali.
Kwa mantiki hiyo, ushindi wa Bokai umeweka historia nchini humo kwa kuwa mtu wa pili kukirudisha chama tawala cha zamani madarakani na ushindi wake ni wa kisasi dhidi ya Weah ambaye alimshinda katika uchaguzi uliofanyika mwaka 2017.