Wakati Afrika inazihesabu siku chache kuifikia Oktoba 22 mwaka huu ambayo tuzo kubwa za muziki barani Afrika maarufu kama MAMAs (MTV Africa Music Awards 2016) zitafanyika  jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini, mtangazaji wa 100.5 Times FM, Omary ‘Lil Ommy’ Tambwe anatarajia kuweka kambi jijini humo.

Mtangazaji huyo wa kipindi cha The Playlist ameiambia Dar24 kuwa lengo la kuweka kambi jijini humo akihudhuria utoaji wa tuzo hizo ni kurusha moja kwa moja taarifa zote muhimu zinazohusu tuzo hizo hadi kufikia siku ya kilele chake, kupitia kipindi hicho maarufu kinachokuwa hewani kila Jumamosi, saa 6 hadi saa 8 mchana kupitia redio hiyo.

“Kama unavyojua Tanzania tunashiriki tuzo hizo tukiwakilishwa na Navy Kenzo, Diamond Platinumz, Vanessa, Raymond, Yamoto Band. Kwa hiyo ni siku muhimu kwetu wadau wa muziki na nataka fans wapate zaidi ya kile wanachotarajia,” alisema Lil Ommy.

“Nitafanya mahojiano ana kwa ana na wasanii wakubwa barani Afrika na kuripoti taarifa mbalimbali za kipekee kuhusu tuzo hizo kabla, wakati na baada ya tuzo. Itakuwa ya kibabe sana,” aliongeza.

Tambwe amekuwa akisifika  kwa uwezo wake mkubwa wa kufanya mahojiano na watu maarufu ndani na nje ya nchi hususan kwenye upande wa burudani.

Diamond Platinumz, Salama Jabir, AY, Joh Makini ni baadhi ya wasanii ambao waliwahi kukiri kuwa walifaidika na kukubali ujazo wa mahojiano waliyofanya kwenye The Playlist na mtangazaji huyo.

“Yaani umeniuliza maswali ambayo huwa natamani siku moja niulizwe lakini sehemu nyingi nimepita hawajawahi kuniuliza. Naomba nikiri kuwa interview ilikuwa kali, nimependa sana,” Diamond alikaririwa baada ya kufanya mahojiano na Lil Ommy.

Kwa live updates na taarifa kuhusu tuzo za MAMAs 2016, unaweza kum-follow kwenye mitandao yake ya kijamii, Twitter, Instagram, Facebook, Periscope kwa jina la @LilOmmy pamoja na YouTube channel yake ni LilOmmytv.

Jamvi La AFCON 2017 Lakunjuliwa, Herve Renard Apewa Mtihani
Jaji Lubuva aomba wananchi kutoa ushirikiano elimu ya mpiga kura