Waziri Mkuu wa Zamani ambaye pia alikuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chadema anayeungwa mkono na Ukawa, Edward Lowassa ameweka wazi msimamo wake na Ukawa kuhusu mustakabali wake kisiasa, hali ya Zanzibar pamoja na uchaguzi uliopita kwa ujumla.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Lowassa alieleza kuwa bado hajakata tamaa kufuatia kushindwa katika uchaguzi mkuu uliopita bali ataendeleza mapambano ya kisiasa akiwa na chama chake pamoja na Ukawa.

“Nitaendelea kuwa imara kwenye siasa, I might have lost the battle not the war (inaweza kuwa nilishindwa pambano sio vita),” alisema Lowassa.

Lowassa aliongeza kuwa vyama vya upinzani vinavyounda Ukawa vinaendelea kupinga matokeo ya urais wa Jamhuri ya Muungano yaliyompa ushindi Dkt. John Magufuli kwa madai kuwa matokeo ya uchaguzi huo yalichakachuliwa waziwazi na ushahidi wanao. Alisema ushahidi huo watauweka hadharani wakati muafaka utakapofika ili watanzania waweze kufahamu kilichofanyika.

“Wakati muafaka utakapofika tataweka bayana ushahidi huo ili Watanzania wajue kwa nini Ukawa inasema kwa dhati kuwa haitambui matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi na kwanini hatutashirikiana na serikali ya sasa ambayo ni batili kisheria,” alisema.

“Kama sheria ingeruhusu tungeenda mahakamani kupinga uamuzi wa Tume ya Uchaguzi. Uamuzi huo umetekelezwa tu kwa sababu ya fitna ya Sheria mbovu zilizotungwa kuhakikisha CCM inabaki madarakani milele. Hii lazima tuendelee kuikataa na kupinga kwa nguvu zetu zote,” aliongeza.

Lowassa alitaka wananchi kuendelea kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu kwa utulivu na amani bila kufanya maandamano ya aina yoyote.

Ingawa alikataa kueleza mbinu atakazozitumia katika kuendeleza mapambano yake kisiasa kwa madai kuwa hawezi kuweka silaha zake hadharani, alisisitiza kuwa Ukawa itaendeleza mapambano ndani na nje ya Bunge na kwamba wataipigania Katiba ya Wananchi ili iweze kutumika.

Hata hivyo, Lowassa alikataa kueleza endapo wabunge wa Ukawa watahudhuria hotuba ya Rais John Magufuli au la akidai kuwa itafahamika wakati utakapofika, “tutavuka mto tutakapoufikia.”

Akizungumzia msimamo wa Ukawa kuhusu hali ya kisiasa visiwani Zanzibar na uamuzi wa mwenyekiti wa ZEC kufuta matokeo, Lowassa alieleza kuwa viongozi wa umoja huo walifanya mkutano Novemba 9 mwaka huu na kuweka msimamo wao kuwa hawakubaliani na tamko la mwenyekiti huyo.

“Wakuu  wa Ukawa walikataa dhana kuwa uchaguzi uleule unaodaiwa kufutwa kwa kuwa ulikuwa na mizengwe, ulizaa matokeo halali kwa wabunge Bunge la Jamhuri ya Muungano na Rais wa Jamhuri, lakini batili kwa wajumbe wa Baraza la wawakilishi na Baraza la Zanzibar,” alisema.

“Hii ina maana kuwa hata ushindi unaodaiwa na Dkt. Magufuli, mbali ya kuwa ni matokeo ya wizi kwa kura za Tanzania bara, pia ni batili kisheria kwani hana ridhaa ya watu wa pande zote mbili za Muungano,” alisema mwanasiasa huyo mkongwe.

Alisisitiza kuwa Ukawa wanaitaka ZEC kumtangaza haraka Maalim Seif Sharif Hamad kuwa rais wa Zanzibar kama matokeo yanavyoonesha kuwa alishinda.

 

Polisi watumia mabomu Hospitali ya Bugando Kuwatawanya Chadema
Samwel Sitta, Dkt. Nchimbi wakatwa Rasmi Uspika, Hawa ndio wamepitishwa