Jeshi la polisi mkoani Mwanza jana lililazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wafuasi wa Chadema waliofurika katika hospitali ya Bugando kwa lengo la kuuona mwili wa mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Geita, Alphonce Mawazo aliyeuawa kwa kukatwa na panga juzi.

Duru kutoka mkoani humo zinaeleza kuwa wafuasi wa Chadema kutoka mikoa mbalimbali ya kanda ya ziwa walifika katika hospitali hiyo wakiwa na msafara wa magari zaidi ya 50 huku wakiimba nyimbo za chama hicho.

Wafuasi hao walitaka kuruhusiwa na walinzi ili waingie kuuona mwili wa Mawazo lakini walinzi waliwaeleza kuwa wanaweza kuruhusu magari mawili pekee kuingia, uamuzi ambao waliupinga na kushinikiza kuingia wote.

Bugando

Kufuatia sintofahamu hiyo, walinzi wa hospitali hiyo waliita Jeshi la Polisi ambalo baada ya kufika katika eneo la tukio na kushindwa kuelewana na wafuasi hao, lililazimika kupiga mabomu kuwatawanya hali iliyozua taharuki kwa wagonjwa na wakazi wa eneo linalozunguka hospitali hiyo.

“Tumefanikiwa kudhibiti vurugu hizo, ni suala la kutoelewana tu, taratibu za hospitali ya rufaa Bugando ziko wazi, walitaka kulazimisha vitu ambavyo haviwezekani. Tumewakamata baadhi na tunaendelea kuwahoji,” alisema Mkuu wa Upelelezi wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Augustine Senga.

Alphonce Mawazo aliuawa kikatili kwa kukatwa na panga kichwani mkoani Geita katika mazingira ambayo yanasadikika kuwa ya kisiasa. Polisi Mkoani Geita jana ilitangaza kuwa inawashikilia watu wanne wanaoaminika kuwa walishiriki kutekeleza tukio hilo.

Diamond Afunika AFRIMMA, Vanessa Naye Ang'ara
Lowassa afunguka Kuhusu Msimamo Wa Ukawa Kuhusu Matokeo na Anachofanya Baada ya Kushindwa