Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amemwaga wino kutoa mtazamo wake ikiwa ni mwaka mmoja tangu Watanzania waliposhiriki uchaguzi mkuu uliompa ushindi, Dkt. John Magufuli kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kupitia waraka wake huo, Lowassa ambaye alikuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya Chadema akiungwa mkono na vyama vya upinzani vilivyounda Ukawa, amekosoa mwenendo wa Serikali ya CCM akieleza kuwa hivi sasa maisha yamezidi magumu na kwamba ahadi ya elimu bure haitekelezwi kama ilivyotarajiwa.

“Pamoja na mafanikio machache katika baadhi ya maeneo lakini maisha yamezidi kuwa magumu, ajira imeendelea kuwa bomu linalosubiri kulipuka, Elimu bure iliyoahidiwa siyo inayotekelezwa,utumishi wa umma umekuwa kaa la moto,” Lowassa ameandika.

“Nasononeka sana nikiona viongozi wanavyoshindana kuwasweka ndani madiwani na viongozi wengine wa kuchaguliwa hasa wa UKAWA,” ameongeza.

Aidha, Mwanasiasa huyo mkongwe ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chadema aliwashukuru wapiga kura waliomuunga mkono katika uchaguzi uliopita huku akisisitiza kuwa hivi sasa ana ari na nguvu kuliko kipindi chote kilichowahi kutokea.

Lowassa aliandika barua hiyo jana (Oktoba 25), tarehe ya mfanano wa siku ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana ambao ulitajwa kuwa uchaguzi wenye ushindani mkubwa zaidi kuwahi kutokea tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini.

Uchambuzi wa kiuchumi juu ya mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Tano, unaonesha kuwa pato la taifa limezidi kuongezeka, makusanyo ya kodi yamepaa, uchumi umekuwa kwa asilimia 7.2 lakini deni la taifa pia limezidi kupaa.

 

Rais Magufuli aongoza kwa kishindo kinyang’anyiro cha tuzo ya Forbes
Wayne Rooney Ashauriwa Kufuata Nyayo Za Gerrard, Lampard