Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amepiga marufuku wanafunzi wanaoanza darasa la kwanza kutokuandikishwa mpaka wazazi wao walipe michango wanayodaiwa katika shule mbalimbali jimboni kwake Mwibara, Wilayani Bunda, Mkoa wa Mara.

Lugola ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mwibara, amemtaka Afisa Elimu wa Kata ya Chitengule, Jimboni humo, Thadeo Lukinisha kuruhusu shule za msingi zilizopo katika Kata yake kuandikisha wanafunzi hao bila kikwazo chochote kwakuwa elimu ya shule ya msingi ni bure nchi nzima.

Lugola amepiga marufuku utaratibu huo ambao amesema hauna msingi wowote kwasababu unawaonea watoto ambao hawana kosa lolote hata kama kuna madeni ambayo wazazi wa wanafunzi hao wanadaiwa kutokana na watoto wao wanaoendelea na masomo katika shule zilizopo jimboni humo.

“Huu utaratibu sio sawa, haukubaliki, kipindi hiki wanafunzi wanaandikishwa kuanza darasa la kwanza waandikishwe bila kikwazo chochote ili waweze kupata elimu yao kama inavyostahili, michango yenu haihusiani na wanafunzi kuanza shule,” amesema Lugola.

Hata hivyo, Afisa Elimu huyo amekiri kutokea kwa tukio hilo, lakini akasema kuwa walifanya hivyo kutokana na baadhi ya wazazi kutolipa kiasi cha shilingi mia nne ambayo inachangwa kwa ajili ya kila mwanafunzi anachangia kwa ajili ya kumlipa mpishi pamoja na mafuta ambayo fedha hiyo inalipwa kwa mwaka.

 

UKAWA waungana na CCM, sasa kuongoza jiji la Dar kwa zamu
JPM aagiza fedha za sherehe ya uhuru zikajenge 'Uhuru Hospital' Dodoma