Wakati Tanzania ikiendelea kufaidika na mapinduzi ya teknolojia ya huduma za kutuma na kupokea fedha kwa njia ya simu, M-Lipa ambao ni mfumo ulioundwa na kampuni ya kitanzania, DataVision International unawawezesha wafanyabiashara kufanya makusanyo na kutuma fedha kwa njia mbalimbali za kielektroniki, umeongezwa thamani kwa kuunganishwa na KwikPay kwa lengo la kurahisisha zaidi huduma hiyo.

Meneja wa M-Lipa, Magori Kihore amesema kuwa ushirikiano huo umelenga katika kuhakikisha kuwa wafanyabiashara, walaji na wananchi kwa ujumla wanapata suluhisho bora zaidi na rahisi zaidi la njia za kufanya malipo ya kielektroniki ili kuendana na lengo laa Benki Kuu ya Tanzania la kuongeza matumizi ya njia za kieletroniki katika kufanya malipo.

“Muunganiko wa mfumo wa M-Lipa na KwikPay unalenga katika kuleta mgawanyo bora zaidi wa utoaji huduma ili kuwezesha huduma jumuishi ya malipo iliyo ya uhakika na haraka wakati wote. Tunaamini kwa hakika kuwa kupitia KwikPay wateja wetu watapata urahisi zaidi wa kufanya malipo kwa ajili ya walaji wa huduma zao wakati wote,” amesema Bw. Kihore.

Akielezea ufanisi wa KwikPay, Paschal Giki ambaye ni kiongozi wa mfumo huo, amesema ni mfumo wa teknolojia inayomsaidia mtumiaji kuruka hatua ya USSD ya kawaida ya kufikia malipo ya fedha kwa njia ya simu.

“Ukiwa na KwikPay, wafanyabiashara wanaotumia M-Lipa wanawawezesha wateja wao kufanya malipo kwa njia salama zaidi na haraka zaidi kwa kutumia hatua chache kupitia QR Code na kuruka hatua za USSD,” amesema Giki.

Hatua ya uboreshaji wa miundombinu ya kutuma na kupokea fedha kwa njia ya kielektroniki yanayowezeshwa na mapinduzi ya TEHAMA, unaakisi dira ya miaka mitano ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli ya kuboresha maisha ya wananchi kwa kutumia TEHAMA.

Katika hotuba yake ya kufungua Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Magufuli alisema kwakuwa shughuli nyingi duniani zinafanyika kwa kutumia TEHAMA, Serikali yake itatoa kipaumbele kwenye ubunifu wa TEHAMA, kuboresha matumizi ya simu za mkononi ili kupatikana nchi nzima, na kuongeza matumizi ya mitandao kutoka 43% ya sasa hadi 80%.

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Novemba 22, 2020
NBC Bukoba yatoa msaada Tani 4 za Saruji