Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba amesema maadhimisho ya miaka 78 ya Umoja wa Mataifa yatafanyika Oktoba 24, 2023 katika Viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam na kwamba Tanzania inajivunia kuwa mwanachama wa Umoja huo.

Makamba ameyasema hayo kupitia mwakilishi wake Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Noel Kaganda na kusema Tanzania imekuwa ikifanya vizuri katika baadhi ya maeneno ya malengo ya maendeleo endelevu hususan katika masuala ya chakula, elimu, jinsia, nishati, maji, amani na usalama.

Balozi kaganda ameongeza kuwa, Tanzania inajisikia fahari kama mwanachama wa UN kwa kusimamia kikamilifu misingi ya Umoja huo na kuendelea kutoa mchango wake katika kutekeleza malengo adhimu huku Mratibu Mkazi wa UN Tanzania, Zlatan Milišić akisema UN inafurahia kuadhimisha miaka 78 tangu kuanzishwa kwake.

Aidha, amesema pia wanafurahi miaka 62 ya ushirikiano kati yake na Tanzania ambapo wakati wote zimekuwa na uhusiano mzuri na imara na Tanzania imekuwa ikichangia kikamilifu katika kuchagiza ajenda ya maendeleo ya kimataifa, katika kuandaa na kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).

Maadhimisho ya mwaka huu yataongozwa na kaulimbiu isemayo “Kuwekeza leo kwa ajili ya kesho kwa kuinua vijana wa Kitanzania”. Maadhimisho hayo yataongozwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki.

Watumishi 11 wasimamishwa kazi Dodoma
Victor Osimhen kuwekwa sokoni SSC Napoli