Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad ameeleza kushangazwa na maelezo ya Mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba kuhusu waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa.

Lowassa alihama CCM na kujiunga na Chadema, kisha kugombea urais akiungwa mkono na vyama vya siasa vinavyounda Ukawa, CUF kikiwa kimojawapo.

Mwanasiasa huyo amedai kuwa yeye hakuwa na wazo la Lowassa bali aliletewa na Profesa Lipumba ambaye aliliwasilisha hadi katika mkutano mkuu wa chama hicho na likaridhiwa, hivyo anashangaa kumsikia akidai kuwa chama hicho kinataka kuuzwa kwa Chadema.

“Profesa Lipumba ndiye aliyemleta Lowassa Ukawa, iweje leo aseme CUF inataka kuuzwa kwa Chadema? Kama mwenzangu anageukageuka kama kinyonga mimi siwezi,” Maalim Seif anakaririwa na Mwananchi.

Aliongeza kuwa Profesa Lipumba ambaye alipendekeza jina la ‘Ukawa’ wakati wa Bunge la Katiba Mpya, ndiye aliushawishi umoja huo kumualika Lowassa akieleza kuwa ingawa amekuwa akisemwa sana, ndiye mtu ambaye wananchi wanamtaka zaidi kwa wakati huo.

Profesa Lipumba alitangaza kujiuzulu nafasi yake ya Uenyekiti wa chama hicho miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana akipinga uamuzi wa kumpa nafasi Lowassa kugombea urais akiungwa mkono na Ukawa. Alichukua uamuzi huo siku chache baada ya kuonekana mbele ya waandishi wa habari akimtambulisha Lowassa na kumkaribisha ndani ya umoja huo.

Kutoka Maktaba

Kutoka Maktaba

Hata hivyo, Profesa Lipumba alirejea mwaka huu na kudai kuwa ametengua uamuzi wake wa kujiuzulu na anarudi kwenye nafasi yake, hali iliyozua mgogoro mkubwa ndani ya chama hicho na kupelekea kufungua kesi mahakamani.

Aidha, Maalim Seif ambaye hivi sasa ana mgogoro wa kutomtambua Profesa Lipumba kama Mwenyekiti wa chama hicho, amedai kuwa tofauti kati yake na msomi huyo ni kwamba yeye ana msimamo wa kile anachokizungumza.

“Tofauti yangu na Profesa Lipumba ni kwamba nikifanya maamuzi nimefanya. Sirudi nyuma. Sina mambo ya kugeukageuka, siwezi nikauweka ulimi wangu kwenye pua. Hii ndiyo tofauti yetu kubwa,” anakaririwa.

Katika hatua nyingine, Maalim Seif amezisifu juhudi za Rais John Magufuli za kupambana na rushwa na ufisadi. Mwanasiasa huyo mkongwe amewaka wananchi kumuunga mkono Rais Magufuli katika jitihada hizo za kuokoa mali za umma na kurejesha uwajibikaji kazini.

Gari la Sugu lilivyochukua maisha ya mtoto yatima
Mwana Fa afunguka kuhusu wimbo wa Darassa ‘kuzipa shida’ hits za wasanii wakubwa