Serikali imetoa zaidi ya shilingi Bilioni 3 kwa mwaka 2022 ili kuwanufaisha vijana katika kazi zao za kimaendeleo na kuanzisha miradi au biashara.

Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Patrobas Katambi, amesema hayo katika kikao kilichoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani, UNFPA kwa ajili ya kutoa mukhtasari kwa waandishi wa habari kuelekea kilele cha siku ya vijana kimataifa.

“Vijana ndio chachu ya Mabadiliko yeye tija ya kisayansi, vina ndio nguvu kazi ya Taifa, hivyo serikali imewekeza katika vijana kwa upande wa sera na sekta zote kama Kilimo na biashara,” amesema Katambi.

Amesema Serikali kupitia Ilani ya CCM inayosema Vijana wawezeshwe inatoa elimu kwa kila kiongozi wa eneo husika juu ya utoaji wa fedha hizo na namna ya kuzipata, kuzitumia kwa malengo ya kimaendeleo ili ziweze kuwanufaisha vijana husika na sio watu wengine ambao sio vijana.

“Vijana wengi wanachukua fedha na kubadilisha malengo, hili linasababisha kunakuwa na ule msemo wa kukopa harusi kulipa matanga, na kwa sababu hiyo fedha hizo zinakuja kupotea bila kurejeshwa, au zikikaa, muda mrefu bila kuchukuliwa na vijana unakuta makundi mengine yanajigawia.” Naibu waziri Katambi.

Awali akimkaribisha Mgeni rasmi kuzungumza na waandishi wa habari Naibu Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu Duniani, UNFPA, Dr. Wilfred Ochan , alisema Vijana wana mchango mkubwa kwa Maendeleo ya Ulimwengu na hivyo jamii nzima inathamini na kufahamu umuhimu wao.

“Ulimwenguni kote, Vijana husema, ‘hakuna chochote chetu, bila sisi’ UNFPA tumesikia, tumejifunza na kutilia maanani kauli hii, ushirikiano wetu na vijana ni lazima kila wakati uwe, kulingana na ushiriki wao wa dhati,” alisema.

“Tanzania ni sehemu ya Jumuia ya Kimataifa, na hivi sasa mataifa yanajiandaa na siku ya vijana ambayo inatukumbusha umuhimu wa vijana na pia kutumia nguvu kazi katika kujenga maendeleo ya Dunia na nchi. Tunataka Vijana wajue kuwa tunawajali na tunawathamini kwa michango yao ya kimaendeleo,” amesema Dr Ochan.

Mmoja wa vijana wanaojikita katika kuwasaidia vijana, Diana Rose aliwapa ujumbe vijana kuhakikisha wanachukua hatua kuhakikisha wanajikwamua kiuchumi, kuwa na afya bora na kuhakikisha kila mahali kuna mazingira salama kwa Maendeleo ya Vijana.

Kauli mbiu katika siku ya Vijana Kimataifa iliyotafsiriwa kuendana na mukktadha wa Nchi ya Tanzania ni ‘Kila Mmoja anahusika katika kujenga uchumi Imara, Ustawi na Maendeleo endelevu, Jiandae Kuhesabiwa.’ na kwa Tanzania Maadhimisho haya yatafanyika jijini Dar Es Salaam Agosti 12.

Rais Samia: Afrika inahitaji juhudu zaidi kwenye Soka
Mama kizimbani kwa mauaji ya kimada wa mumewe