Majina ya watumishi 138 wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi yamewasilishwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa ajili ya uchunguzi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mawasiliano ya Wizara hiyo, Waziri anayesimamia wizara hiyo, William Lukuvi alimuagiza Katibu Mkuu wa Wizara kuwasilisha Takukuru majina ya watumishi hao.
Lukuvi aliwasimamisha kazi watumishi hao kwa tuhuma za kuingilia mfumo wa ukadiriaji wa kodi ya ardhi, hatua inayodaiwa kuisababishia Serikali hasara.
Ingawa Waziri Lukuvi alipotangaza hatua hiyo hakutaja kiasi cha hasara iliyosabaishwa, Naibu Waziri wa wizara hiyo, Angeline Mabula amesema kuwa ni mabilioni ya fedha.
“Zinafahamika, ni bilioni za fedha na zinangoja uchunguzi, siwezi kukupa kiasi kamili,” alisema Naibu Waziri huyo.
“Tukimaliza uchunguzi ndio tutajua ni kiasi gani. Lakini ni mabilioni ya pesa,” aliongeza.