Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amewafungia kwa muda wa miezi mitatu madereva 10 wa mabasi ambao wamekuwa wakikiuka sheria ya usalama barabarani kwa kuendesha kwa mwendo wa kasi.
Pia ameliagiza Jeshi la Polisi nchini kupitia kikosi cha usalama barabarani kuwachukulia hatua madereva hao ikiwa ni pamoja na kuwapeleka mahakamani kwa makosa hayo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, jijini Dodoma, Simbachawene amewataja madereva hao kuwa ni Allan Msangi ambaye huendesha gari lenye namba za usajili T605 DJR kutoka Kampuni ya Kapricon ambalo hufanya safari zake katika Mikoa ya Dar-Moshi na hutembea kwa Km 125 kwa saa.
Waziri huyo amemtaja dereva mwingine ni Hussein Dudu kutoka kampuni ya Kimotco Intertrade ambaye huendesha gari lenye namba za usajili T520 CXE ambalo hufanya safari katika Mikoa ya Arusha na Musoma na hutumia mwendokasi wa Km 126 kwa saa.
Mwingine ni Selemani Selemani ambaye huendesha gari lenye namba za usajili T 313 DSO kutoka kampuni ya Al Saedy ambalo hufanya safari zake katika njia ya Dar – Kilombero na hutumia mwendokasi wa Km 103 kwa saa.
Dereva mwingine ni Athumani Mzava ambaye huendesha gari lenye namba za usajili T 391 kutoka kampuni ya MB Coach ambalo hufanya safari zake katika njia ya Dar- Arusha na hutumia mwendokasi wa Km 107 kwa saa.
Mbali na hao kuna, Juma Simba wa gari lenye namba T 340 DPW la Kampuni ya Baraka Classic ambalo hufanya safari zake kati Dar- Masasi na hutumia mwendokasi wa Km 107 kwa saa.
Wengine ni, Salum Salum wa Kampuni ya Maning Nice, Frank Masawe wa Machinga, Innocent Thomas wa Esta Luxury, Nassoriv Nassoro wa NBC Classic na Michael Mkinda wa Kilimanjaro Express.
“Kwa Mamlaka niliyonayo nawafungia madereva hawa kwa muda wa miezi mitatu. Nawaagiza wamiliki wa mabasi haya ambayo madereva wamekiuka sheria ya usalama barabarani kuhakikisha wanachukua hatua stahiki kwa madereva wao,” amesema Waziri Simbachawene.