Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewataka wanaotoza kodi kwa wafanyabiashara waache kutumia nguvu zaidi bali watumie akili katika ukusanyaji wa kodi.

Rais Samia ametoa agizo hilo kwa Wizara ya Fedha wakati akizungumza baada ya uapisho wa Viongozi mbalimbali uliofanyika Ikulu, jijini Dodoma leo Aprili Mosi 2021.

“Trend mnayokwenda nayo sasa mnaua Walipakodi, mnaua Wafanyabiashara, mnatumia nguvu zaidi kuliko akili na maarifa kupata kodi, sasa wale mnaowakamua mkienda mkachukua vifaa vya kazi, mkafungia akaunti zao na kuchukua pesa kwenye akaunti, akitoka anafunga biashara anahamia Nchi ya Pili,” amesema Rais Samia.

“Mnaua Wafanyabiashara (kwa kutumia nguvu kukusanya kodi) mnapunguza walipa kodi, nendeni mkatengeneze na kutanua wigo wa walipa kodi, yale mengine yanayowapunguzia watu ari ya kulipa kodi Waziri (Mwigulu Nchemba) naomba ukayasimamie,” amesisitiza Rais Samia.

Naye Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amezitaka Wizara zote kusimamia vizuri mapato na kuhakikisha yanaongezeka huku akiweka bayana dhamira ya Serikali kutaka kufikia makusanyo ya Shilingi Trilioni 2 kwa Mwezi.

“Mheshimiwa Waziri wa Fedha, kabla ya mwisho wa mwaka huu tuwe tumefikia Wastani wa Shulingi Trilioni Mbili kwa Mwezi, inawezekana, mkajipange vizuri, na kwa upande wa TAMISEMI vivyo hivyo, Mheshimiwa Ummy, huko kuna kazi kubwa, kuna kazi ya mapato, lakini kuna kazi ya kudhibiti matumizi, haya mkayasimamie Wizara zote,” amesema Dkt. Mpango.

Aidha, Rais Samia amegongelea msumari dhamira hiyo iliyowekwa bayana na Makamu wake Dkt. Mpango ambapo amesema, “Waziri wa Fedha (Mwigulu Nchemba) umepewa kigezo hapa cha Trilioni mbili kwa Mwezi, tunataka Trilioni mbili kwa Mwezi muende mkatanue wigo wa kodi lakini pia mkatengeneze walipa kodi wengi zaidi,” amesisitiza Rais Samia.

Mjumbe Simba SC amkingia kifua 'Mo'
Cavani kubaki Man Utd