Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameliegiza Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha kufanya maamuzi ya kupima ardhi haraka na kutenga maeneo kwa ajili makazi na viwanda ili kujiandaa na uwekezaji mkubwa.

Majaliwa ametoa agizo hilo mapema leo Novemba 19, 2016 wakati akizungumza na wananchi na viongozi mbalimbali wa Serikali na wa Mkoa wa Pwani mara baada ya kukagua kiwanda cha kutengeneza magari ya zimamoto na matrekta cha Equator SUMA JKT Limited kilichopo Ruvu JKT, wilayani Kibaha mkoani Pwani.

Majaliwa amesema ujenzi wa kiwanda hicho utakuwa mkombozi kwa taasisi nyingi na Halmashauri nyingi nchini kwani zilikuwa zinashindwa kumudu bei ya kununua magari ya zimamoto.

Amesema baadhi ya Halmashauri nyingi zilikuwa zinanunua gari moja kwa sh. milioni 500 na hiki ni kiasi kikubwa mno, kwa hiyo kiwanda hicho kitakuwa mkombozi kwa taasisi nyingi na halmashauri zetu.

Pia amesema kuwa ameguswa kukuta kiwanda hicho pia kina uwezo wa kutengeneza matreka na zana za kilimo (farm implements) kwani asilimia kubwa ya Watanzania ni wakulima na wanategemea jembe la mkono. “Kupitia kiwanda hiki, matrekta mengi yataunganishwa na nina imani bei itakuwa ya chini ili wananchi waweze kumudu.”

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Equator SUMA JKT Ltd, Eng. Robert Mangazini amemweleza Waziri Mkuu kwamba asilimia 80 ya ujenzi wa kiwanda hicho imekamilika na kwamba hivi sasa wako kwenhye hatua ya kufunga mitambo. Hata hivyo, alisema wanaisubiri iwasili kutoka India.

Amesema kiwanda hicho kikikamilika kitaweza kuunganisha matrekta 3,000 kwa mwaka na magari ya zimamoto 100 na kubainisha kuwa faida za kuunganisha magari hayo hapa nchini ni kuwa na uwezo wa kuzalisha vipuri ndani ya nchi.

Kuhusu teknolojia ya utengenezaji wa magari ya zimamoto, Eng. Mangazini alisema kiwanda hicho ni cha pili kujengwa barani Afrika cha kwanza kikiwa huko Bassa, Afrika Kusini.

Man Utd, Arsenal watoshana misuli, Mourinho aendeleza 'mwiko' wake
Sakata la Mchezaji Langa Lesse Bercy Wa Jamhuri ya Congo laishtua tena TFF