Maendeleo ya Afya ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu yanahitajika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam ambapo kesi dhidi yake na wenzake inasikilizwa.
Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba amewataka wadhamini wa mbunge huyo kufika mahakamani hapo kueleza maendeleo yake kiafya baada ya Wakili wa Serikali Mwandamizi, Patrick Mwita kuwasilisha ombi hilo jana.
“Kesi hii imekuja kwa ajili ya kuendelea lakini hadi sasa hatuna taarifa ya hali ya mshtakiwa wa nne (Lissu), tunaamini hata Mahakama hii haina rekodi ya maendeleo yake,” wakili Mwita alisema.
Hakimu Mkuu Simba alikubali ombi hilo na kueleza kuwa hata yeye hafahamu hali ya mtuhumiwa huyo ingawa amekuwa akimuona kwenye televisheni.
Lissu amekuwa nje ya nchi kwa matibabu tangu Septemba 7, 2017 baada ya kushambuliwa kwa risasi akiwa eneo la nyumbani kwake Area D jijini Dodoma.
Baada ya kutibiwa katika hospitali ya Dodoma, mbunge huyo alisafirishwa kwenda jijini Nairobi ambako alitibiwa hadi Januari mwaka 2018 alipohamishiwa nchini Ubelgiji alipo hadi sasa.
Katika kipindi cha hivi karibuni, amekuwa akifanya mahojiano na vyombo vya habari vya kimataifa na kufanya ziara katika mataifa kadhaa kwa lengo la kukutana na viongozi wa nchi hizo pamoja na vyombo vya habari.
Lissu amekuwa akieleza kuwa daktari wake amemruhusu kusafiri katika maeneo ya jirani kwani bado anaendelea na matibabu yake ingawa hali yake imeimarika.