Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, imepokea fedha zaidi ya Shilini 60 Bilioni ndani ya siku 730 za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, zilizoelekezwa kusaidia uinuaji wa sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, kilimo, uvuvi na taasisi za serikali.
Akizungumza na Viongozi na wananchi, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Muleba, Justus Magongo amewataka Mkurugenzi na Watendaji kusimamia utekelezaji wa miradi, ili kufikia malengo ya ilani ya Chama Cha Mapinduzi – CCM.
Amesema, ”tunaendelea kutekeleza miradi mbalimbali na hapa sio kwamba tumefikia asilimia 100 bado kazi inaendelea, Mkurugenzi tuendelee kusimamia kazi hizi, lakini pia fedha zinazotoka serikali kuu tuendelee kuzisimamia vizuri ili wananchi hawa waendelee kupata huduma.”
Awali, akitoa taarifa juu ya miradi iliyotekelezwa katika kipindi cha miaka miwili ya Rais Samia Madarakani, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, Elias Kayandabila alisema fedha hizo zimeelekezwa katika taasisi za Serikali, ujenzi wa Hospitali ya Wilaya na ujenzi wa vyumba 457 vya madarasa.
Amesema “fedha zilizotolewa kutoka kwa Rais zimewezesha ujenzi wa hospitali ya wilaya ambayo haikuwepo na ujenzi wa madarasa mapya 457.”