Mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa yameendelea kuzibomoa nyumba nchini Sudan wiki hii, huku idadi ya vifo ikiongezeka na kufikiwa watu 66 tangu kuanza kwa msimu wa mvua nchini humo.
Mapema wiki hii, mamlaka za Serikali nchini humo, ilisema watu 50 walipoteza maisha tangu kuanza kunyesha kwa mvua mwezi Juni.
msemaji wa Baraza la Kitaifa la Ulinzi wa Raia la Sudan, Brigedia Jenerali Abdul-Jalil Abdul-Rahim Agosti 16, 2022 alisema kuwa takriban watu 28 waliripotiwa kujeruhiwa katika kipindi hicho kutokana na mvua hizo zinazoendelea kunyesha.
Mashuhuda nchini humo, wanasema zaidi ya nyumba 24,000 yakiwemo majengo ya serikali yameharibiwa vibaya au kuharibiwa kabisa na kwamba umakini unahitajika katika suala la utoaji misaada kwa kujali pande zilizoathiriwa zaidi.
Sudan, imekuwa ikiendeshwa bila Serikali inayofanya kazi tangu mapinduzi ya kijeshi ya Oktoba, yaliyovuruga kipindi cha mpito cha muda mfupi cha kidemokrasia, kufuatia kuondolewa kwa kiongozi wa muda mrefu wa Taifa hilo Omar al-Bashir mwaka wa 2019 katika uasi wa wananchi.
Takwimu za Tume ya Misaada ya Kibinadamu, inayoendeshwa na Serikali ya nchi hiyo imesema kwa ujumla, takriban watu 136,000 wameathiriwa na mvua kubwa na mafuriko katika majimbo 12 kati ya 18 ya Sudan.
Msimu wa mvua nchini Sudan kwa kawaida huanza mwezi wa Juni na hudumu hadi mwisho mwa mwezi Septemba, huku mafuriko yakishika kasi mwezi Agosti na Septemba.
na zaidi ya watu 80 kufariki katika matukio yanayohusiana na mafuriko wakati wa msimu wa mvua kwa mwaka jana pekee.
Mwaka wa 2020, mamlaka za nchi hiyo zilitangaza Sudan kuwa eneo la janga la asili na kuweka hali ya hatari ya miezi mitatu kote nchini humo, baada ya mafuriko na mvua kubwa kuua watu wapatao 100 na kusomba zaidi ya nyumba 100,000.