Rais John Magufuli ameeleza kuwa hatua anazozichukua dhidi ya watu wanaohujumu na kufanya ubadhirifu wa rasilimali za umma hazihusiani na udikteta bali ni dhamira yake ya kutaka kila mwananchi kufaidi keki ya taifa.

Rais Magufuli aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam katika kilele cha Siku ya Sheria nchini, alipokuwa mgeni rasmi  katika uzinduzi wa Mwaka wa Mahakama uliohudhuriwa na Jaji Mkuu, Othman Chande.

Alisema kuwa wapo baadhi ya watu wanaocheza na fedha za serikali kwa namna wanavyotaka huku wananchi wengine wakiwa katika umasikini uliokithiri. Hivyo, aliitaka Mahakama kuharakisha uanzishwaji wa kitengo cha ufisadi ili kutoa hukumu kwa kesi zinazohusu wizi na ufisadi kwa kasi ili kuokoa fedha za umma na kuzuia wabadhirifu wanaendelea kuitafuna keki ya taifa.

“Kwahiyo ninapojaribu kuchukua hatua ndugu zangu, Mheshimiwa Jaji Mkuu na Waheshimiwa Majaji… mimi sio kichaa, sio mnyama, mimi sio dikteta. Lakini angalau nataka nifanye sadaka yangu angalau kwa kipindi nitakachokuwa naishi hapa duniani, inawezekana hata baada ya kufa nitakuwa Rais kule wa malaika kidogokidogo,” alisema Rais Magufuli huku akiwaacha wahudhuriaji na vicheko.

Rais Magufuli pia alionesha kushangazwa na ripoti zinazoonesha kuwa India na Kenya ndio wanaoongoza kwa uuzaji wa madini ya Tanzanite duniani ili hali madini hayo adhimu yanapatikana Tanzania peke yake.

“Mmenichagua kuwa Rais wa Tanzania, huu mkate unaopatikana… bila kujali dini zetu, makabila yetu, vyama vyetu wote wafaidike na hii rasilimali ambayo watanzania tunaipata,” alieleza Rais Magufuli.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli aliahidi kuipa kada ya Mahakama kiasi cha shilingi bilioni 12.5 walizoomba ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa muda huku akiahidi kuwaongezea mishahara wafanyakazi wa Mahakama nchini katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/17.

Rais Magufuli alimuomba Jaji Mkuu, Othman Chande kumpa majina ya Mahakimu waliotekeleza ipasavyo majukumu yao na kutoa hukumu ya kesi zaidi ya 900 kwa wakati uliopangwa ili awaandikie barua ya kuwapongeza, ikiwa ni hatua ya kuwatia moyo kwa kazi nzuri waliyoifanya.

 

 

Beyonce amtumbua jipu meneja wake
Waliomdhalilisha Mtanzania India watiwa Mbaroni, Hofu yaongezeka