Rais John Magufuli amewataka watanzania na wanasisa kwa ujumla kuachana na siasa kwa sasa hadi ifikapo wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2020, akiwataka kujikita katika kufanya kazi.

Rais Magufuli alitoa kauli hiyo jana alipopokea ripoti ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kutoka kwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Damian Lubuva.

“Niwaombe wanasiasa wenzangu, tufanye siasa za ushindani kwa nguvu zote baada ya miaka mitano ili wananchi watuhoji tuliyoyaahidi, tuliyoyatekeleza au hatukuyatekeleza,” alisema Rais Magufuli.

Alisema kuwa hivi sasa, siasa zinazotakiwa kufanyika ni zile za wawakilishi waliochaguliwa na wananchi ambao wanapaswa kuzifanya katika Mabaraza ya madiwani na Bungeni pekee wanapowawakilisha wananchi.

“Kila nchi, hata zenye demokrasia, unapokwisha uchaguzi, mnakuwa wachapa kazi, haiwezekani mkawa kila siku ni siasa, watu watalima saa ngapi,” alihoji Rais Magufuli.

Kauli ya Rais Magufuli imekuja kukiwa na vuguvugu la mvutano kati ya vyama vya upinzani na Jeshi la Polisi lililopiga marufuku mikutano ya kisiasa kwa sababu walizodai ni za kiusalama.

Jeshi hilo pia lilizuia kufanyika kwa makongamano ya Bajeti yaliyoandaliwa na Chama Cha ACT-Wazalendo pamoja mahafali ya wanafunzi wa Chadema.

Baada ya kauli ya Rais Magufuli, Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe aliandika kupitia ukurasa wake wa Facebook kuipinga akitaka vyama vya Siasa kuungana dhidi ya kile alichokiita vita dhidi ya Demokrasia.

Zitto aliandika:

Kauli ya Rais ya Kuzuia Vyama vya Siasa Kufanya Shughuli za Siasa kwa Miaka Mitano ni Tangazo la Vita dhidi ya Demokrasia na Mfumo wa Vyama vingi Nchini

Tumepokea kwa MSHTUKO na masikitiko makubwa kauli ya Rais kwamba vyama vya siasa havipaswi kufanya siasa isipokuwa wakati wa Kampeni na kupitia bungeni. Kimsingi kauli ya Rais ni kauli yenye nia ya kuvunja Sheria ya Vyama vya siasa inayolinda uwepo wa mfumo wa vyama vingi na kuhimiza vya vya siasa kufanya shughuli za siasa katika msimu wote ili kuthibitisha uhai wao.

Tunaichukulia kauli ya Rais kama tangazo la vita dhidi ya demokrasia na uhai wa vyama vingi nchini. Chama chetu kitaitisha vikao vya dharura kujadili hali ya siasa nchini na namna ya kukabiliana na mashambulizi yanayoendelea dhidi ya demokrasia nchini mwetu.

Tunatoa wito kwa vyama vyote vya siasa vinavyoamini katika misingi ya demokrasia nchini kukutana haraka na kujadili namna ya kuunganisha nguvu pamoja katika kupigana vita mpya ya kulinda demokrasia nchini mwetu.

Aidha, tunatoa wito kwa wananchi wote na taasisi za kiraia kusimama imara katika kulinda demokrasia. Tunasisitiza kuwa ushahidi wa kisayansi duniani kote unaonyesha kuwa huwezi kuua demokrasia bila kuua juhudi za maendeleo. Tusiruhusu mtu yeyote mwenye mamlaka kuua demokrasia nchini mwetu.Hatua zozote za kuua demokrasia ni kuua Umoja, Amani na Mshikamano wa wananchi na Taifa, ambayo ndiyo misingi ya maendeleo ya nchi yetu kijamii, kisiasa na kiuchumi. Tunatoa wito kwa wananchi wote kushikamana na kusimama imara katika kipindi hiki kigumu ili kulinda demokrasia.

Shomari Kapombe, Pascal Wawa Wafanyia uchunguzi Wa Kiafya
Video: 'Nipo pamoja na wanasiasa na atashirikiana nao vyema' - Rais Magufuli