Serikali ya awamu ya Tano imefanikiwa kuwatia nguvuni magwiji wa biashara ya dawa za kulevya waliokuwa wanawaweka rehani watanzania wenzao huko ughaibuni na kupewa ‘unga’ kuuleta nchini kwa mali kauli.

Kamanda wa Polisi kanda maalum ya Dar es Salaam, Simon Siro aliwaaambia waandishi wa habari jana jijini humo kuwa watu hao wanaoshikiliwa na jeshi hilo, ni wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya waliokuwa wanafanya biashara hiyo kupitia mataifa mbalimbali.

Aliwataja watu hao kuwa ni Mohamed Abdallah Omary mwenye umri wa miaka 37, mfanyabiashara na mkazi wa jiji la Dar es Salaam ambaye alikuwa anawaweka rehani watanzania wenzake nchini Pakistan na kupewa mzigo wa ‘unga’ kwa mali kauli.

Mwingine ni Nassoro Suleiman mwenye umri wa miaka 35 ambaye ni Meneja wa duka moja la kubadilishia fedha. Alisema mtu huyu alikuwa anatumia duka lake liliko jijini Dar es Salaam, kushirikiana na genge la wauzaji wa dawa za kulevya kubadilisha fedha na kusafirisha kiasi kikubwa cha fedha kwa njia zisizo halali.

“Lakini waandishi wa habari, uchunguzi umebaini kuwa sababu kuu ya ongezeko la matumizi ya dawa za kulevya ni kushamiri kwa mitandao ya kimataifa ya wahalifu wa madawa ya kulevya wanaoshirikiana na watanzania kufanya biashara ya kusafirisha binadamu kwenda nchi za uzalishaji wa dawa za kulevya hususan nchi za kiarabu na kuwaweka rehani ili wapatiwe kiasi kikubwa cha dawa za kulevya kwa mali kauli,” alisema Kamanda Siro.

 

Wahariri wa Mawio wahojiwa na Polisi kwa Saa Nne, Jukwaa la Wahariri lapanga kumkataa Nape
Msajili wa Vyama vya siasa awajibu BAVICHA, asema amewachukulia hatua CCM