Kesi ya Kikatiba ya kupinga Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa wa Mwaka 2018 iliyofunguliwa na kiongozi wa Chama Cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe na wenzake wawili leo imetupiliwa mbali na Mahakama Kuu ya Tanzania.
Zitto, Joram Bashange (Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi – CUF upande wa Bara), Salim Bimani (Mkurugenzi wa Uenezi, Habari na Mahusiano wa CUF), walifungua kesi hiyo kwa niaba ya vyama 10 vya upinzani dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Katika shauri hilo, walalamikaji waliiomba Mahakama Kuu kutangaza kuwa kifungu cha 8(3) cha cha Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi kuwa kinakiuka Katiba (unconstitutional). Walieleza kuwa kifungu hicho kinachozuia muswada kupingwa mahakamani kinapaswa kutangazwa kuwa kinakiuka Katiba.
Katika ombi lao la pili, Zitto na wenzake waliiomba Mahakama hiyo kuzuia Muswada huo kuwasilishwa Bungeni kwa madai kuwa unakiuka haki za msingi kwa kufanya shughuli nyingi za kisiasa kuwa kosa la jinai; pia walidai kuwa unampa Msajili wa Vyama vya Siasa Mamlaka Makubwa na kuingilia shughuli za ndani za vyama vya siasa.
Akitoa uamuzi wa shauri hilo, Jaji Benhajj Masoud alikubaliana na hoja kadhaa za Serikali za kupinga maombi ya Zitto na wenzake, akieleza kuwa shauri hilo linachanganya maombi mawili kwa pamoja.
Aidha, Jaji Masoud alikubaliana na hoja nyingine ya upande wa Serikali iliyoeleza kuwa Shauri hilo linakiuka kifungu cha 8(2) cha Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi na Wajibu.
Jopo la Mawakili wa Serikali liliongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Mark Mulyambo na Jopo la Mawakili wa upande wa akina Zitto liliongozwa na Mpare Mpoki.
Akizungumza baada ya uamuzi huo wa mahakama, Zitto amesema kuwa anaheshimu maamuzi ya mahakama lakini wataendelea kudai haki hiyo kupitia njia ya Mahakama.
“Mahakama ndio sehemu ya haki. Sisi tutaendelea tu kuja Mahakamani, hatutaacha kupigania haki hii. Mkumbuke kwamba mwaka huu tumeutangaza kupitia Azimio la Zanzibar kuwa ni mwaka wa kudai Demokrasia,” alisema Zitto.
“Kwahiyo tutadai demokrasia kwenye Nyanja zote. Kama mnavyoona Jaji ametoa uamuzi wake na ndani ya muda huohuo tumeshaagiza shauri lingine lifunguliwe kwa sababu ni lazima tuendelee kupigania haki, na Mahakama ni moja ya eneo ambalo tunaamini kabisa kwamba haki inaweza kupatikana na inaweza kutendeka,” aliongeza.