Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewakaribisha viongozi wa kiwanda cha kusindika samaki aina ya Jodari kuja nchini kuangalia maeneo ya uwekezaji wa viwanda vya samaki.

Amesema Serikali imeweka sera nzuri za uwekezaji na pia ina maeneo mengi na mazuri kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda vya samaki, ambayo ni bahari, mito na maziwa ambayo aina mbalimbali za samaki.

Majaliwa amesema hayo wakati alipotembelea kiwanda cha samaki cha Mer des Mascareignes kilichoko jijini Port Louis nchini Mauritius.

“Tanzania kuna fursa nyingi za uwekezaji hasa kutokana na mazingira yake. Mnaweza kuja kuwekeza kwenye viwanda vya usindikaji wa samaki tuna bahari, mito na maziwa yenye samaki wa aina mbalimbali,” alisema.

Amesema Serikali imedhamiria kuimarisha uchumi wake kupitia sekta ya viwanda ili kuongeza tija kwa Taifa na kwa wananchi kiujumla hivyo wanahitaji wawekezaji waliotayari kuja kuwekeza nchini.

Akizungumzia suala hilo, Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Khalid Salum Mohammed alisema Tanzania inahitaji wawekezaji watakaowekeza kwenye uvuvi wa kina kirefu na ujenzi wa viwanda vya samaki.

Amesema lengo la uwekezaji huo ni kukuza uchumi wa Taifa pamoja kupanua soko la ajira na kuondoa umaskini miongoni mwa wananchi wake.

Na kwa upande wake Meneja Mkuu wa kiwanda hicho, Patrick Hill alisema wamefurahi na mualiko wa kuja Tanzania kwa ajili ya kuangalia fursa na uwekezaji na kwamba wako tayari kushirikiana na Serikali.

Amesema kampuni yao inajishughulisha na usindikaji wa samaki aina moja tu ya jodari na wananunua kutoka kwa makampuni makubwa ya uvuvi huku wateja wao wakubwa wakiwa ni bara la Ulaya.

Tanzania na China zasaini mkataba wa utamaduni
Thibaut Courtois Aigwaya Real Madrid