Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Nape Nnauye pamoja na Naibu Waziri wa Utamaduni kutoka Jamhuri ya  watu wa China, DONG WEI wamesaini programu ya utekelezaji wa Mkataba wa masuala ya Utamaduni wa miaka mitatu kuanzia mwaka 2017 hadi 2020 leo Jijini Dar es Salaam.

Nape amesema kuwa Mkataba huo unalengo la kuimarisha  na kuendeleza ushirikiano katika Sekta ya Utamaduni ambao umedumu kwa miaka mingi ulioasisiwa na Baba wa Taifa Mwl.Julius K. Nyerere.

“Tanzania na China tumekuwa na ushirikiano wa muda mrefu wa masuala mbalimbali ikiwemo hili la Utamaduni ambalo limetumika kukuza, kulinda na kuunganisha nchi zetu kuwa kitu kimoja”, Amesema Nape.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Utamaduni wa China, DONG WEI amesema kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na China uliokuwepo kwa muda mrefu  katika masuala  ya Utamaduni, Sanaa, Elimu,Ngoma na  Michezo yamesaidia kuimarisha ushirikiano uliopo na kuwezesha nchi hizi mbili kunufaisha katika maeneo hayo.

Hata hivyo, Mkataba huo pamoja na mambo mengine una lengo la kuendeleza na kufanya mpango wa pamoja kwa siku za usoni, kufanya matokeo makubwa katika Sekta ya Utamaduni kati ya nchi hizo mbili, Kufanya mkutano maalum wa ushirikiano wakati muafaka, kuzidisha ushirikiano kwenye sekta ya viwanda katika bidhaa za Utamaduni na Kubadilishana wataalamu na mafunzo ya kiutamaduni.

 

Andres Iniesta: Siendi Popote
Majaliwa akaribisha wawekezaji kuja nchini