Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amekagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa Daraja la mawe katika barabara ya Iguguno-Kikhonda-Kinampundu, lenye urefu wa mita 30.
Waziri Mkuu amefanya ukaguzi huo hii leo Julai 17, 2022 na kuwapongeza wakandarasi waliofanikisha usimamizi na ujenzi wa daraja hilo kwa ufanisi.
Ujenzi wa daraja hilo, ni sehemu ya kazi zilizofanyika katika Mkataba wa Matengenezo ya muda maalumu ya barabara ya Mwando – Miganga – Kinandili, yenye urefu wa kilomita 12.39.
Aidha, mara baada ya Waziri Mkuu kuwapongeza wakandarasi hao kwa ubunifu wa daraja hilo, pia ameagiza wapewe kazi ya ujenzi wa madaraja mengine.
Awali, Meneja wa TARURA mkoa wa Singida, Mhandisi Tembo David amesema ujenzi wa daraja hilo utasaidia kuondoa changamoto ya mawasiliano iliyokuwepo kwa wananchi hasa kipindi cha masika.
Daraja hilo limejengwa kwa kutumia teknolojia rahisi ya mawe kwa gharama ya shilingi milioni 102.