Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Afisa Mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Liwale, Omary Chingwile ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Liwale na kuviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi juu ya tuhuma hizo.

Waziri Mkuu amemsimamisha kazi mtumishi huyo wakati akizungumza na madiwani, watumishi na wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Liwale akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Lindi.

Majaliwa amesema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amesisitiza matumizi mazuri ya fedha za umma ili zikamilishe miradi ya maendeleo ya wananchi na kwamba Serikali haitamvumilia mtumishi yoyote anayetumia vibaya fedha za umma.

“Hatuwezi kufanya mchezo na fedha ya Serikali. Tunahitaji kila mradi uende vizuri, fedha iliyoletwa lazima itumike kama ilivyokusudiwa.”

“Waheshimiwa madiwani, Halmashauri yenu inakusanya mapato hadi asilimia 100 lakini hatujawahi kuona mradi wowote unaotekelezwa na halmashauri na ukawa wa mfano.”

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Liwale, Judith Nguli kufuatilia fedha za wakulima wa korosho na ufuta ambao hawajalipwa na vyama vya ushirika abavyo vilikusanya mazao yao.

“Nakupongeza Mkuu wa Wilaya kwa kuchukua hatua ya kumsimamisha kazi Afisa Ushirika, Bw. Ephraim Kipomela kutokana na upotevu wa fedha za ushirika usiishie hapo hakikisha vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama vinafanya uchunguzi na kubaini namna fedha hizo zilivyopotea,”.

Awali, akikagua ujenzi wa nyumba za wafanyakazi wa Magereza, Waziri Mkuu amempongeza Mkuu wa Magereza wa Liwale, Gilbart Sindani kwa ubunifu wa kuanzisha mradi wa uuzaji wa mbao jambo lililowezesha gereza hilo kujiendesha na kujenga majengo mapya ya utawala pamoja na nyumba za wafanyakazi.

Wangeona mafunzo mlionayo wasingethubutu - IGP Sirro
Taifa Stars kuifuata Benin leo