Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kusimamia weledi, kanuni na taratibu zilizowekwa kwenye kila sekta ya utumishi wa umma na kwamba pale patakapojitokeza uvunjifu wa maadili na miiko iliyowekwa, hatua stahiki za kinidhamu zitachukuliwa.
Majaliwa ameyasema hayo hii leo (Alhamisi, Februari 2, 2023) wakati akitoa taarifa kuhusu masuala ya ukatili shuleni katika Kikao cha Tatu cha Mkutano wa 10 wa Bunge, Bungeni jijini Dodoma, iliyolenga kufafanua changamoto ya nidhamu na malezi ya wanafunzi na adhabu zinazotolewa shuleni.
Amesema, mesema shule zimekuwa kioo cha malezi ya watoto katika kusimamia na kujenga nidhamu katika jamii na jukumu hilo limekuwa likitekelezwa na walimu na wazazi kwa lengo la kuwajenga watoto hasa wanapokwenda kinyume na nidhamu, ambapo viboko hutumika kama moja ya adhabu ya kuwarejesha katika mstari.
“Hivi karibuni tumeshuhudia kupitia vyombo vya habari, vitendo vya adhabu kali dhidi ya wanafunzi kwa baadhi ya shule zetu. Adhabu hizo zimefanywa na baadhi ya walimu walio na mafunzo ya kutosha ya malezi, mahali pengine Mwalimu Mkuu mwenye dhamana ya kuongoza shule, ambaye anafahamu utaratibu wa utoaji wa adhabu shuleni.” amesema Waziri Mkuu.
Aidha, Majaliwa pia ametoa wito kwa walimu wakuu na wakuu wa shule kutumia walimu wa malezi, ushauri na unasihi pamoja na Viongozi wa Dini katika kuwarekebisha watoto na kuwajenga kimaadili ili kuepukana na matumizi ya adhabu ikiwemo viboko.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema wazazi na jamii wanapaswa kushirikiana kwa karibu na walimu katika kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao ya kuwafundisha, kuwalea, kuwaongoza na kuwaendeleza wanafunzi kimwili, kiakili na kiroho kwa uadilifu na kwa kuzingatia sheria, mila, desturi na tamaduni za Kitanzania.