Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewasimamisha kazi Maofisa Misitu wanne na kusimamisha shughuli za uvunaji wa mazao ya misitu wilayani Rufiji kwa muda usiojulikana baada ya kutoridhishwa na usimamizi wake.

Majaliwa amesema kuwa hakuna mafanikio katika sekta ya misitu kwenye wilaya ya Rufiji.

“Nasimamisha shughuli zote za uvunaji wa mazao ya misitu pamoja na watendaji wake kwa sababu hatuwezi kuacha watu wanakata magogo bila ya kufuata taratibu,” – Majaliwa

Majaliwa amefanya uamuzi huo leo Septemba 26, 2016 wakati akizungumza na watumishi wa wilaya ya Rufiji kwenye ukumbi wa halmashauri kabla ya kuzungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara kwenye viwanya jumba la maendeleo wilayani Rufiji.

Maofisa hao waliosimamishwa kazi ni pamoja na Mkuu wa Idara ya Ardhi, Maliasili na Mazingira Dk. Paul Ligonja, Ofisa Misitu wilaya Gaudens Tarimo, Ofisa Misitu Yonas Nyambuya na Ofisa wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) wa wilaya Seleman Bulenga.

Waziri Mkuu pia amemuagiza Mkuu wa Wilaya hiyo, Juma Njwayo kukusanya magogo yoye yaliyoko msituni na kuyapiga mnada na kuitaka  wizara ya Maliasili na Utalii kwenda wilayani Rufiji kufanya uchunguzi wa leseni za uvunaji walizozitoa kwa wilaya hiyo.

“Haiwezekani Rufiji iwe shamba la bibi, nimesimamisha uvunaji wa magogo hata kwa wenye leseni hadi tuzichunguze zimetoka wapi. Hatuwezi kuruhusu maofisa wanashiriki vitendo vya hujuma kwa kuvuna misitu Rufiji na kugonga mihuli ya Kilwa kisha fedha wanatia mifukoni,”- Majaliwa.

 

Akiri mahakamani kufanya mauaji yaliyomfunga jela pacha wake kwa kufananishwa
Mtoto: Natamani ningekuwa smart phone